KIVUKO CHA MV. MAFANIKIO KUREJEA MTWARA BAADA YA WIKI TATU

News Image

Posted On: July 22, 2021

Huduma za Kivuko kwa wakazi wa Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara zinatarajiwa kurejea baaada ya takribani wiki tatu kutoka sasa, hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle leo wakati alipotembelea eneo la Yadi ya Songoro Marine kukagua maendeleo ya ukarabati huo unaofanywa na kampuni ya Songoro.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kukagua ukarabati wa kivuko hicho Mtendaji Mkuu Maselle amesema kivuko hicho kipo mbioni kukamilika kwani Mkandarasi ametakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda mfupi ili wakazi wanaotegemea kivuko hicho Mkoani Mtwara waweze kurejeshewa huduma zake mapema iwezekanavyo.

‘’Tumekisafirisha kivuko hiki kutoka Mtwara kuja hapa Dar es salaam kwakuwa ni gharama ndogo kukileta hapa kuliko kusafirisha vifaaa vyote vyamatengenezo kwenda kufanyia Mtwara ndio maana mkandarasi akaamua kukivuta kivuko hiki kije hapa ili muda wa matengenezo uwe mfupi zaidi’’.

Mhandisi Maselle amesisitiza kuwa utaratibu wa kufanya matengenezo kwa vivuko vya TEMESA ni muhimu sana kwa vyombo vya maji kwakuwa maji ya bahari yana chumvi nyingi na kali hivo kama kivuko kitakuwa hakijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu kitakuwa kinaharibika na kitashindwa kufanya kazi kwani chuma chake kitaliwa na maji ya chumvi na hivyo kushindwa kudumu kwa muda mrefu.

‘’Ni utaratibu wa kawaida kwa TEMESA kila ambapo kivuko kinafikia muda wake wa matengenezo kinga, lazima kitolewe na kupelekwa kufanyiwa ukarabati na matengenezo na hii ni hatua mojawapo ambayo tumefanya na tunaendelea na ukarabati wa vivuko vingine ambavyo muda wake wa ukarabati umefika’’. Alisema Mhandisi Maselle ambapo amewaomba wakazi wa Mtwara wavumilie wakati kivuko hicho kikiendelea kufanyiwa ukarabati ambapo wakazi hao wamepelekewa boti mbili za MV. TANGAZO na MV. KUCHELE ambazo zinatoa huduma kwa sasa kwa wakazi hao.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo la ukaguzi amesema, ukarabati wa kivuko hicho umefikia asilimia 85% na ameongeza kuwa wanatarajiwa kumaliza ukarabati wake ifikapo Tarehe 15 mwezi Agosti.

‘’Kazi kubwa zote tulizozifanya ziko kwenye hatua ya mwisho ili kuweza kukamilisha ukarabati wa kivuko hicho,’’ amesema Songoro.

Kivuko cha MV.MAFANIKIO kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa na tani 50 na kinatoa huduma zake kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara mjini.