MWENYEKITI WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA AIPONGEZA TEMESA KWA UTOAJI HUDUMA BORA
Posted On: July 10, 2026
Mwenyekiti wa Ofisi ya Rais – Tume ya Utumishi wa Umma, Bi. Hamisa Kalombola, ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amejionea huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo. Akiwa katika banda la TEMESA, Bi. Kalombola alipata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na wakala huo, ikiwemo usimamizi na uendeshaji wa vivuko, matengenezo ya magari ya Serikali pamoja na huduma nyingine za kiufundi zinazochangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Baada ya kutembelea banda hilo, Bi. Kalombola aliipongeza TEMESA kwa mchango wake katika utoaji wa huduma muhimu na kuitaka kuendelea kuimarisha ubora wa huduma zake, hususan katika uendeshaji wa vivuko na matengenezo ya magari ya Serikali. “Endeleeni kutoa huduma bora za vivuko na endeleeni kututengenezea magari yetu vizuri,” amesema Bi. Hanusa Hanusi Kalombola.
Naye Katibu Tume ya Utumishi wa Umma, Nolasco J. Kipanda ameipongeza TEMESA kwa kazi kubwa inazoendelea kuzitekeleza.
Kwa upande wake, Fundi Mkuu kutoka TEMESA Abdul Malambo ameueleza ujumbe huo kuwa, TEMESA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi, sambamba na kuboresha huduma zake ili kuendelea kukidhi matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla.
TEMESA ni wakala wa Serikali wenye jukumu la kutoa huduma za ufundi na umeme, ikiwemo matengenezo ya magari na mitambo, usimamizi wa vivuko, pamoja na huduma nyingine za kiufundi zinazounga mkono utoaji wa huduma za umma.