KAMISHNA JENERALI WA MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA ATOA WITO KUIMARISHWA KWA USIMAMIZI WA KISHERIA WA HUDUMA ZA VIPANDO (LIFT)
Posted On: July 08, 2026
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa kazi za usimamizi wa huduma za matengenezo ya vipando (Lift) katika majengo ya Serikali kwa kulipa jukumu hilo hadhi ya kiudhibiti ili kuongeza usalama wa wananchi na kudhibiti shughuli zinazofanywa na watu wasio na sifa stahiki.
Kamishna Lyimo alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo alipata maelezo kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na TEMESA, hususan ukaguzi, matengenezo na usimamizi wa lVipando (ifti) ambapo amesema ipo haja ya kutafakari namna ya kuimarisha sheria inayosimamia huduma hizo ili kuhakikisha zinatekelezwa na wataalamu wenye sifa na weledi unaotakiwa hasa kutoka taasisi za Serikali kama TEMESA.
Kamishna Lyimo ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti ongezeko la watu wasio na utaalamu wanaojihusisha na huduma za Vipando (lifti) (vishoka), kulinda usalama wa watumiaji, kuongeza uwajibikaji kwa watoa huduma na kuhakikisha viwango vya kitaalamu vinafuatwa katika ukaguzi na matengenezo ya lifti nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa kitengo cha Masoko na Uhusiano kutoka TEMESA Bi Martha Joachim ameeleza kuwa TEMESA itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za kihandisi kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, huku ikiendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuimarisha mifumo ya usalama na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.