MITATU YA DODOMA NA SAMIA: UBORESHAJI WA KARAKANA YA MKOA NA USIMIKAJI MIFUMO YA UMEME MJI WA SERIKALI MTUMBA DODOMA.
Imewekwa Monday 13th May , 2024
MITATU YA DODOMA NA SAMIA: UBORESHAJI WA KARAKANA YA MKOA NA USIMIKAJI MIFUMO YA UMEME MJI WA SERIKALI MTUMBA DODOMA.
UTANGULIZI:
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ni Wakala chini ya Wizara ya Ujenzi ulioanzishwa chini ya mamlaka ya sheria ya wakala za serikali Na. 30 ya mwaka 1997 kwa amri ya serikali na Waziri wa Ujenzi kupitia tangazo la serikali Na. 254 la tarehe 26 Agosti 2005.
TEMESA ilianzishwa mahususi kutoa huduma za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali katika karakana ambazo zipo kila Mkoa Tanzania Bara, kufanya matengenezo na usimikaji wa mifumo ya Umeme, mabarafu, viyoyozi na Elektroniki inayomilikiwa na Serikali, uendeshaji na usimamizi wa vivuko vya Serikali, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali na Umma kwa ujumla katika Nyanja za uhandisi mitambo, umeme na elektroniki na ukodishaji wa Mitambo ya ujenzi.
Wakala unaendesha na kusimamia karakana 27 zilizopo katika Mikoa yote Tanzania Bara na karakana tatu ngazi ya Wilaya ambazo zinatoa huduma ya matengenezo ya magari, pikipiki, mitambo na kutoa huduma za ushauri na usimikaji wa mifumo ya umeme na viyoyozi katika majengo ya Serikali yaliyopo katika Mikoa yote Tanzania Bara.
Aidha, Wakala unaendesha na kusimamia vivuko 32 vya Serikali vinavyotoa huduma maeneo mbalimbali kote Nchini.
Wakala pia umefanikiwa kukamilisha ujenzi wa jengo lake jipya la Makao Makuu hapa Mkoani Dodoma na kuhamia ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais za kuhakikisha ofisi zote za Zerikali zinahamia Dodoma kamaMakao makuu ya Nchi.
Pamoja na kutekeleza majukumu yake ya msingi, Wakala unaendelea kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 67,723,669,790.20 na USD 7,043,765 ambayo inajumuisha ujenzi wa vivuko na maegesho, ukarabati wa vivuko na maegesho, Ujenzi na ukarabati wa Karakana na uanzishwaji wa Karakana mpya katika Mikoa mipya.
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeendelea kuboresha huduma zinazotolewa na Wakala kwa kufanya maboresho makubwa ili kuhakikisha unatoa huduma iliyo bora yenye tija na ya uhakika kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla.
Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 katika utoaji wa huduma za Wakala kwa Mkoa wa Dodoma ni kama ifuatavyo:
- Katika kipindi cha Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imeweza kutoa zaidi ya shilingi Bilioni 7.2 ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa karakana mpya na ukarabati. Mkoa wa Dodoma ni mojwapo ya mnufaika wa fedha hizo kwakuwa Serikali kupitia TEMESA imeanza mchakato wa usanifu wa karakana mpya na ya kisasa ambayo itajengwa katika maeneo ya Kizota Mkoani Dodoma. Karakana hiyo inatarajiwa kuwa ya kisasa ambayo itaweza kuhudumia magari yote ya Taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kwa ufanisi mkubwa. Kwa sasa iko katika hatua za usanifu chini ya mtaalamu Chuo cha Adhi.
- Kwa upande wa ukarabati wa karakana ya Mkoa Dodoma, mkandarasi tayari amekwishapatikana ambaye ni M/S Wagerasi Investment Ltd kutoka Dar es Salaam na mkataba umekwisha sainiwa wenye thamani ya kiasi cha Shilingi Milioni 973,747,589.96 pamoja na VAT. Mkandarasi huyo anatarajiwa kuanza kazi muda si mrefu ili kuboresha utoaji huduma katika karakana yetu ya Mkoa Dodoma.
- Aidha, katika kipindi cha Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia, Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kununua vitendea kazi vipya, karakana ya Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa karakana ambazo zimefaidika kwa kupata vitendea kazi hivyo vilivyogharimu kiasi cha shilingi Milioni 545,827,514.20 ambavyo vinaendelea kutumika na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa karakana hiyo.
- Wakala pia umekuwa ukiwapeleka kwenye mafunzo wataalamu wake ikiwemo mafundi ili waweze kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kutokea mara kwa mara kwenye magari
Aidha, ili kuendelea kuboresha huduma za karakana, mwezi Novemba, 2023, timu ya maofisa kutoka TEMESA walishiriki katika mkutano wa ushirikiano kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu sekta ya ujenzi uliofanyika hapa Dodoma ambapo TEMESA na Wakala wa karakana Kuu ya Magari Zanzibar waliingia mashirikiano katika kuwajengea uwezo mafundi kuhusu masuala ya ufundi na matengenezo ya magari.
- Aidha, Katika kipindi cha Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia, kwa upande wa Umeme, viyoyozi, majokofu, TEHAMA na Elektroniki, Serikali pia imekuwa ikitoa vitendea kazi kila mwaka na imekuwa ikifanya hivyo ili kuhakikisha TEMESA inapata vitendea kazi vya kisasa na kuweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yanaendelea kujitokeza. Kikosi cha Umeme Kanda ya Kati Dodoma, kimefaidika kwa kupatiwa vitendea kazi kwa ajili ya kutekeleza kwa urahisi na ufanisi majukumu yake ya kila siku ya kusimika mifumo ya TEHAMA na Umeme na elektroniki katika majengo mapya ya Serikali yanayoendelea kujengwa katika mji wa Serikali Mtumba Mjini Dodoma.
Wakala umeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme hapa Mkoani Dodoma ikiwemo kusanifu na kusimika mifumo ya umeme, mifumo ya TEHAMA na mifumo ya viashiria moto, mifumo ya lifti, kangavuke pamoja na mifumo ya upozaji hewa katika majengo mbalimbali yanayoendelea kujengwa katika Makao Makuu ya Nchi Dodoma.
Aidha, Wakala pia kupitia kitengo cha Huduma za Ushauri (TEMESA Consultancy Service Unit) imekuwa ikishiriki katika kufanya kazi za usanifu na kutoa ushauri wa kitaalamu na kusimamia majengo yanayoendelea kujengwa katika Mji wa Serikali (Magufuli City) ulioko Mtumba mjini Dodoma yakiwemo majengo ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Madini, Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Tume ya Madini.
Wakala kupitia Kikosi chake cha Umeme, unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya usimikaji wa mifumo hiyo katika majengo yanayoendelea kujengwa likiwemo jengo la Wizara ya Ujenzi ambapo usimikaji wa mifumo ya umeme mpaka sasa umefikia zaidi ya asilimia 73% pamoja na jengo la Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo usimikaji wa mifumo hiyo umefikia zaidi ya asilimia 98%.
- Miaka Mitatu ya Dodoma na Samia pia inaenda na mabadiliko ya Kiteknolojia na Wakala haujakaa mbali na suala la Teknolojia, Wakala umeweza kutekeleza na unaendelea kutekeleza miradi ya Usimikaji wa Mifumo ya Kielekroniki. Katika ofisi zake za Makao Makuu Dodoma, umesimikwa mfumo wa kufuatilia mapato yanayokusanywa katika vivuko Nchi nzima kwa kutumia mfumo wa Point of Sales) POS.
- Aidha Mfumo wa kusimamia matumizi ya mafuta katika Vivuko na mfumo wa ukusanyaji mapato Kigongo-Busisi unaendelea kuboreshwa. Gharama zilzizotumika katika kusimika mifumo hiyo ni jumla ya shilingi Bilioni 5.9.
- Wakala unatekeleza miradi hiyo ya usimikaji wa mifumo ya kielektroniki kwa lengo la kuboresha Utendaji kazi wa Wakala na kuweka uwazi katika shughuli za Wakala ikiwemo suala la ukusanyaji wa mapato.
Fedha zote zilizotumika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo ni fedha za ndani zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA Ndg. Lazaro N. Kilahala anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo pamoja na kuimarisha utendaji wa Wakala ikiwemo kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika eneo la ujenzi wa vivuko vipya, ujenzi wa karakana mpya na maboresho ya karakana zilizopo ili kuhakikisha TEMESA inaendelea kutoa huduma Bora kwa Fursa za Maendeleo.
Aidha, anaahidi uwekezaji huu wa Serikali utasimamiwa kwa weledi mkubwa huku Wakala ukiendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo na ushauri ili kuendelea kuboresha huduma zake.
MWISHO.
Imeandaliwa na Kitengo cha Masoko na Uhusiano (TEMESA)