ZIARA YA MTENDAJI MKUU LINDI, MTWARA NA RUVUMA
Posted On: March 13, 2019
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle amemaliza ziara yake mikoa ya kusini, mara hii akitembelea mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma ambapo pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi pia alipata fursa ya kukagua usalama wa vivuko vinavyotoa huduma katika maeneo hayo pamoja na karakana za mikoa hiyo.
Akiwa mkoani Lindi Mhandisi Maselle alikagua kivuko cha MV. KITUNDA kinachotoa huduma kati ya Lindi mjini na Kitunda ambapo amezungumza na wafanyakazi wa kivuko hicho na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kivukoni, alipata pia fursa ya kukagua ujenzi wa majengo ya kupumzikia abiria (waiting lounge) pamoja na vyoo vya abiria ambayo yanajengwa na Kikosi cha Ujenzi katika pande zote mbili Lindi na Kitunda ambapo aliridhishwa na kasi ya mkandarasi anayesimamia ujenzi huo na kumtaka ahakikishe anamaliza kazi hiyo kwa uharaka na ubora zaidi.
Mhandisi Maselle pia alipata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi wa karakana ya mkoa pamoja na kukagua na kupokea changamoto zao kiutendaji wanazopambana nazo katika makao makuu ya mkoa huo. Alimuagiza Meneja wa TEMESA mkoa huo Mhandisi Grayson Maleko kuhakikisha mkoa wake unaongeza mapato kwakua umekua haufanyi vizuri katika siku za nyuma
Vile vile Mhandisi Maselle alikagua kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mjini Mtwara na Kivuko cha MV. KILAMBO kinachotoa huduma kati ya Kilambo mjini Mtwara na Namoto Msumbiji. Akiwa katika vivuko hivyo, alisisitiza suala la usalama wa abiria na mali zao ambapo aliwataka mabaharia wanaohudumu katika vivuko hivyo kufanya mara kwa mara mazoezi ya uokozi na pia kutoa elimu kwa abiria hao kuhusu namna ya kujiokoa inapotokea ajali ya kivuko.
Mhandisi Maselle alimaliza ziara yake mkoa wa Ruvuma ambapo alizungumza na wafanyakazi wa wa mkoa huo na kuwapongeza kwa kuwa na wastani mzuri wa mapato kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, aliwataka kuhakikisha mapato yao yanaimarika zaidi kwa mwaka huu wa fedha na kuwaahidi kuzitafutia ufumbuzi kero zao pamoja na changamoto haraka iwezekanavyo.