UFAFANUZI WATOLEWA: WANAFUNZI KIPAUMBELE KUVUSHWA KIGAMBONI

News Image

Posted On: January 12, 2026

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Bw. Moses Mabamba, ametoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu hali ya utoaji wa huduma za vivuko katika eneo la Kigamboni, akibainisha hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wanafunzi wanaorejea shuleni kesho wanavushwa kwa kipaumbele maalum.

Akizungumza leo tarehe 12 Januari 2026 katika eneo la Kivukoni, jijini Dar es Salaam, Bw. Mabamba alisema kuwa kwa sasa kivuko cha MV. KAZI kipo kwenye ukarabati mdogo ambapo tayari injini mbili mpya zimefungwa pamoja na mifumo mipya ya umeme na mifumo mingine ya uendeshaji. Alibainisha kuwa matengenezo hayo yako katika hatua za mwisho na kivuko kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kesho mara baada ya majaribio ya awali kukamilika.

Aidha, Bw. Mabamba alieleza kuwa huduma za uvushaji zinaendelea kutolewa kupitia ushirikiano na wadau wa sekta binafsi – Azam Sea Taxi, ambapo wamekubaliana kuwapa wanafunzi kipaumbele katika huduma hiyo ili kuhakikisha wanawahi shule kwa wakati na kwa usalama.

“Matarajio yetu ni kwamba Serikali imefanya maandalizi makubwa kuhakikisha wanafunzi wanarejea shuleni bila changamoto. Tumewasiliana na wenzetu wa Azam Sea Taxi na wamekubali kushirikiana nasi kuwavusha wanafunzi kwa kipaumbele wakati tukikamilisha majaribio ya MV. KAZI,” alisema Bw. Mabamba.

Aliongeza kuwa ukarabati wa MV. MAGOGONI unaoendelea mjini Mombasa, Kenya, umefikia zaidi ya asilimia 81.3 na kivuko hicho kinatarajiwa kurejea nchini mwezi Aprili 2026. Wakati huo huo, MV. KIGAMBONI kinatarajiwa kumaliza ukarabati mwezi Oktoba 2026. Mara baada ya kurejea kwa vivuko hivyo, TEMESA italipeleka MV. KAZI kwenye ukarabati mkubwa.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha huduma kwa wananchi, hususan wanafunzi, hazikwami na zinaendelea kama kawaida pia amewaomba radhi wananchi kwa usumbufu wowote unaoweza kujitokeza katika kipindi hiki kifupi cha mpito na kuekeza kuwa Serikali, kupitia TEMESA, inafanya kila jitihada kuhakikisha huduma za vivuko zinaimarishwa kwa ufanisi.