MV.KAZI YAONGEZEWA INJINI, KUANZA KAZI LEO

News Image

Posted On: January 13, 2026

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umetangaza kurejea kwa huduma ya kawaida ya kivuko cha MV. KAZI kuanzia leo mchana baada ya kukamilika matengenezo yake madogo yaliyofanyika kwa siku nne.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la Magogoni jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Moses Mabamba alisema matengenezo hayo yamegharimu shilingi milioni 30, fedha zilizotumika kuboresha mifumo muhimu ya uendeshaji wa kivuko hicho.

Alisema kuanzia Januari, 5 mwaka huu, TEMESA na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), walitoa tahadhari ya uwepo wa upepo mkubwa baharini hatua iliyoulazimu Wakala kusimamisha huduma kwa muda kwa sababu za kiusalama.

''Baada ya huduma kusimamishwa, TEMESA ililazimika kuanza matengenezo, tumebadilisha injini mbili zilifungwa ili kushirikiana na injini zilizokuwepo awali, kuboresha mifumo ya umeme na mifumo mingine ya uendeshaji. Kivuko hicho sasa kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 madogo, pikipiki, baiskeli na maguta.'' Alisema Mabamba.

Aidha Mabamba alisema wakati wote ambao kivuko kilikuwa katika ukarabati mdogo, shughuli za uvushaji ziliendelea kutolewa kwa kutumia vivuko vya Azam Sea TAXI. Kuhusu kivuko cha MV. MAGOGONI ambacho kinaendelea kufanyiwa ukarabati huko Mombasa Nchini Kenya, alieleza hadi sasa asilimia 81.3% ya ukarabati wa kivuko hicho imekamilika licha ya awali kupangwa kurejea Aprili, jitihada zinaendelea kufanywa ili kivuko hicho kirejee mapema ndani ya miezi michache ijayo.

Alisema kivuo cha MV. KIGAMBONI kiliondolewa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa na kinatarajiwa kurejea kutoa huduma mwezi Novemba mwaka huu. Aidha alisema baada ya vivuko MV. MAGOGONI na MV. KIGAMBONI kurejea, kivuko MV. KAZI kitaondolewa kwenda kufanyiwa ukarabati mkubwa kwakuwa muda wake wa kufanyiwa ukarabati umefika.

(Uhuru, Januari 13, 2026)