WAZIRI MKUU AAGIZA MALIPO YA HARAKA KUKAMILISHA VIVUKO KIGAMBONI

News Image

Posted On: December 30, 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Mwigulu Nchemba, ameielekeza Wizara ya Ujenzi kuwasiliana kwa haraka na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha inakamilisha malipo ya ujenzi wa vivuko vilivyopo kwenye hatua za ukarabati, kwa lengo la kuviwezesha kurejea kutoa huduma kwa wananchi wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Mhe.Dkt. Nchemba ametoa agizo hilo leo, alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua hali ya utoaji wa huduma ya vivuko katika eneo la Magogoni. Amesema kuwa kukamilika kwa malipo hayo kutaharakisha kurejea kwa vivuko hivyo kazini, hatua itakayosaidia kupunguza kero ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo ya jirani.

“Mhe. Waziri, naomba mwasiliane haraka na Wizara ya Fedha ili fedha zinazohitajika ziweze kutolewa kwa wakati, vivuko hivi vikamilike na virejee kutoa huduma hapa Magogoni,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha, Dkt. Nchemba amesisitiza kuwa malipo hayo yafanyike ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, huku akiwataka viongozi wa sekta husika kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ukarabati huo ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

“Fedha zitakapotolewa, hakikisheni kuwa wakandarasi wanakamilisha kazi kwa haraka. Lengo letu ni kuona vivuko vinarejea mapema kutoa huduma, na hivyo kuondoa changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi wetu,” amesisitiza.

Ziara hiyo imelenga kuonyesha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za usafiri wa majini, hasa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama Kigamboni, na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na kwa wakati.