ZIARA YA KAIMU MTENDAJI MKUU KANDA YA ZIWA

News Image

Posted On: November 07, 2018

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle leo ameendelea na ziara yake ya kutembelea karakana za mikoa na kukagua usalama wa vivuko pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wa wakala huo kwa ujumla.

Mhandisi Maselle akiwa ameongozana na Mkurugenzi Huduma za Ufundi (Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano) Mhandisi Lazaro Vazuri hapo jana walitembelea vivuko vya MV. Sabasaba pamoja na MV. Ukara vinavyotoa huduma kati ya Bugorola na Ukara Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, MV. Ujenzi kinachotoa huduma kati ya Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza na Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara, MV. Mara kinachotoa huduma kati ya Iramba na Majita Wilayani Bunda na Wilaya ya Musoma Vijijini Mkoani Mara, na MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Kinesi Wilayani Rorya Mkoani Mara na Musoma Mjini.

Akizungumza na wafanyakazi hao kwa nyakati tofauti, Mhandisi Maselle aliwasisitizia suala la usalama kupewa kipaumbele kikubwa kwa wakati huu ambapo amewataka kuhakikisha wanazingatia taratibu zote za uendeshaji wa vivuko ikiwemo usalama wa abiria na mali zao. Aidha aliwakumbusha suala la nidhamu kwa viongozi wao wanapokuwa maeneo ya kazi lakini pia aliwaomba kuwa na lugha nzuri kwa abiria wanaotumia vivuko hivyo.

Naye Mhandisi Lazaro Vazuri Mkurugenzi Huduma za Ufundi (Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano), alisisitiza vifaa vya uokozi katika vivuko vyote viwekwe wazi na kuonekana kwa urahisi na abiria lakini pia aliwataka kuhakikisha wanatoa mara kwa mara elimu kuhusu hatua za uokoaji inapotokea dharura ya ajali ya kuzama kwa kivuko au moto.

Mhandisi Maselle anatarajiwa kuendelea na ziara yake Mkoani Mwanza ambapo atatembelea kivuko cha Kigongo Busisi kujionea hali ya usalama na utendaji wake.