WAZIRI KAMWELWE AWAFUNDA MAMENEJA TEMESA

News Image

Posted On: March 13, 2020

Waziriwa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe leo amefanya kikao na menejimenti ya TEMESA pamoja na mameneja wa Mikoa na vituo wa Wakala huo ambapo amewataka kuhakikisha wanajiimarisha ili kuendelea kutoa huduma bora na zinazokidhi viwango.

Akizungumza katika Kikao hicho ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa TEMESA Mkoa wa Dodoma Waziri Kamwelwe amewataka kutekeleza maagizo yote ambayo ameyatoa ikiwemo kupunguza gharama za matengenezo ya magari, kununua vipuri kwa wingi pamoja na kuhakikisha mafundi wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuweza kuendana na teknolojia ya kisasa ya ufundi wa magari.

Aliupongeza Wakala kwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa mwishoni mwa mwaka jana ikiwemo ununuzi wa vipuri wa pamoja (Bulk Procurement), uanzishwaji wa karakana za wilaya ikiwemo karakana ya Kilombero na Kahama pamoja na kuanzishwa kwa karakana inayotembea (mobile workshop).

“Niliagiza vitu vingi lakini kwenye taarifa vitu vingi vimetekelezwa maeneo yanayokuwa ni changamoto ni kazi yangu mimi kuvikumbusha,”alisema Mhandisi Kamwelwe

Waziri Kamwelwe pia aliipongeza TEMESA kwenye upande wa huduma za Vivuko kwa kuendelea kutoa huduma bora na kuzingatia usalama wa abiria na mali zao.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Mhandisi Japhet Maselle akizungumza katika kikao hichoalimueleza Waziri Kamwelwe juu ya changamoto ambazo Wakala unakabiliana nazo hasa kwenye upande wa karakana ikiwemo upungufu wa watumishi hasa upande wa mafundi pamoja na madeni makubwa wanayozidai taasisi mbalimbali za serikali yanayofikia shilingi bilioni 16 ambapo Mhandisi Kamwelwe aliahidi kufuatilia kwanini deni hilo halijalipwa mpaka sasa wakati alishaagiza deni hilo lilipwe.

Mhandisi Maselle pia akizungumza katika kikao hicho alieleza hatua mbalimbali walizochukua katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri katika ziara yake aliyoifanya mwishoni mwa mwaka jana ambapo alielezakuwa mengi yameshafanyiwa kazi ikiwemo kuacha kupeleka magari ya serikali katika karakana za binafsi ambapo ameeleza kuwa yamechangia kukuza pato la TEMESA kwa kiasi kikubwa.

Mhandisi Maselle pia aliishukuru serikali kupitia wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuiamini TEMESA na kuwataka mameneja hao kutilia mkazo maagizo yanayotolewa na viongozi kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma bora kwa serikali na wananchi kwa ujumla.