VIVUKO VIPYA VYAKAMILIKA, KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WAKAZI UKEREWE

News Image

Posted On: March 05, 2026

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imekamilisha rasmi ujenzi wa vivuko vipya viwili kati ya vitano vinavyojengwa na kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard iliyoko mjini Mwanza.

Vivuko hivyo viwili ni MV. UKEREWE kinachokwenda kutoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Nansio Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza pamoja na kivuko MV. BUKONDO kinachokwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Nansio Ukerewe Mkoani Mwanza.

Akizungumza mara baada ya kukagua vivuko hivyo viwili na kuvifanyia majaribio (Sea/ Lake Trial) katika Ziwa Victoria ambako vivuko hivyo vilitembea kwa zaidi ya saa tatu, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa vivuko TEMESA Mhandisi Lukombe King’ombe amesema kuwa kukamilika rasmi kwa ujenzi wa vivuko hivyo viwili kutasababisha kufunguka kwa fursa za kiuchumi na huduma za kijamii kwa wanachi wanaoishi maeneo hayo kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia mitumbwi na boti ndogo za mbao kwa ajili ya kusafiri kutoka eneo moja la kisiwa kwenda eneo jingine hali iliyokuwa ikiwahatarishia usalama wa maisha na mali zao.

Mhandisi King’ombe amesema kuwa adhma kubwa ya timu iliyokwenda kukagua vivuko hivyo viwili kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam DMI na Wizara ya Ujenzi ni kuhakikisha vivuko hivyo viko tayari kwa kuanza kazi ambako wamekagua injini za vivuko hivyo vyote, mitambo na mifumo ya uendeshaji wa vivuko hivyo, vifaa vya uokozi na usalama yakiwemo maboya ya uokozi, boti za dharura za uokozi, mifumo ya kutambua mioto na mifumo ya kuzimia mioto.

“Adhma kubwa ya timu hii kuja kukagua vivuko hivi ni kwa ajili ya maandalizi sasa ya kupekeka vivuko hivi katika maeneo ambavyo vitahudumu, kwahiyo sisi kama timu tumemuwakilisha Mtendaji Mkuu wa TEMESA kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho baada ya vivuko hivi kukidhi vigezo vya ubora kwa maana ya mifumo ya uendeshaji pamoja na vifaa kwa ajili ya usalama wa abiria wanapokuwa ndani ya vivuko.”

Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa vivuko hivyo pia tayari vilipitiwa na kukaguliwa na wataalamu kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na tayari walishatoa vyeti vya ubora ili kuweza kuruhusu vivuko hivyo kwenda kuhudumu katika maeneo ambayo vinapaswa kutumika.

Aidha Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa wamefanya majaribio (Sea/Lake Trial) ya vivuko hivyo na wamejiridhisha kwamba vifaa vyote vya vivuko hivyo vinafanya kazi ambayo ni tayari kwa ajili ya kwenda kuhudumu.

Halikadhalika, timu hiyo ilipata pia wasaa wa kutembelea maegesho ya vivuko hivyo ambayo tayari yamekamilika kwa asilimia kubwa. Mhandisi King’ombe amesema kuwa Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa mindombinu ya maegesho ya vivuko hivyo ambako vivuko hivyo vitakuwa vinapaki kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na mizigo.

“Timu hii pia ilitembelea kwenye maeneo hayo ya maegesho ili kujiridhisha sasa kuwaleta viongozi kwa ajili ya uzinduzi na kupekeka hii huduma kwa wananchi na kufungua fursa za kiuchumi, ni matarajio yetu kwamba vivuko hivi vinakwenda kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi na kuwarahisishia majukumu yao kwasababu katika eneo lile la Bwiro Bukondo wote mnafahamu wananchi wanatumia mitumbwi kwa sasa kwahiyo itakua sasa mitumbwi basi na sasa tunawapelekea vivuko vikafungue fursa kwa wananchi wa maeneo haya.” Alimaliza Mhandisi King’ombe.

Kivuko cha MV. UKEREWE kinao uwezo wa kubeba tani 170, abiria 800 na magari 22 wakati kivuko MV.BUKONDO kinao uwezo wa kubeba tani 100, abiria 200 na magari 10. Vivuko hivyo viwili vimegharimu shilingi Bilioni 11 mpaka kukamilika ujenzi wakena fedha zote zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.