WAZIRI KAMWELWE AKAGUA ENEO LA MRADI WA UJENZI WA KIVUKO KIPYA CHA MAFIA NYAMISATI

News Image

Posted On: August 26, 2019

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amefanya ziara kukagua eneo la mradi wa ujenzi wa kivuko kipya kitakachotoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati. Mradi huo ambao unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.3 za kitanzania.

Zoezi hilo ambalo limefanyika katika yadi ya Songoro iliyopo katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam limeshuhudiwa na Mbunge wa Mafia Mheshimiwa Mbaraka Dau, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA Mhandisi Japhet Maselle, waandishi wa Habari pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya Songoro na wa Wakala huo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mhandisi Kamwelwe alisema wakazi wa Mafia watarajie kupata kivuko hicho ifikapo mwezi Februari mwaka 2020 na ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inamaliza ujenzi wa kivuko hicho kwa wakati kama mkataba unavyosema.

‘’sitarajii kuvuka mwezi wa pili Mheshimiwa Dau, wana Mafia watakuwa wameshapata chombo, tutakipeleka Nyamisati, tutakifanyia majaribio na uone jinsi gani taasisi yangu ya TEMESA inatimiza wajibu wake’’alisema Waziri Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe pia alimtaka Mbunge huyo kuhakikisha wanafuatilia kwa pamoja maendeleo ya mradi huo kwa kutembelea eneo la ujenzi kila baada ya miezi miwili ili kuhakikisha kazi hiyo inamalizika kama ilivyopangwa.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA Mhandisi Japhet Maselle alimsomea Waziri Kamwelwe taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa kivuko hicho ambapo aliishukuru Serikali kwa ufadhili wa ujenzi wa kivuko hicho ambacho kitakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa Nyamisati na Mafia kwani kitawaondolea adha ya usafiri walionayo kwa sasa hasa wananchi wenye kipato cha chini. ‘’Ni lengo la Serikali kutoa usafiri wa uhakika na salama kwa wananchi wake popote pale panapohitajika, tunaishukuru sana Serikali kwa kuiamini TEMESA kuendelea kutekeleza miradi hii lakini pia kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi kama hii ya vivuko kwa lengo la kuboresha huduma za usafirishaji katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu’’, alisema Mhandisi Maselle.

Naye Mbunge wa Mafia Mheshimiwa Mbaraka Dau aliishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo wakazi wa Mafia na kuongeza wanakisubiri kivuko hicho kwa hamu kubwa kwakuwa kitawasaidia kupunguza adha kubwa ya usafiri wanayoipata kwani wanatumia karibu masaa sita kusafiri kwa kutumia majahazi wakati kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa kikitumia masaa mawili na hivyo kupunguza muda wa kusafiri kwa kiasi kikubwa.

Kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 6 sawa na Tani 100.