WATUMISHI WAPYA TEMESA WAASWA KUWA WAZALENDO NA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

News Image

Posted On: November 25, 2025

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala, amefungua rasmi mafunzo maalum kwa watumishi wapya wa wakala huo akiwahimiza kuwa na nidhamu ya hali ya juu, uwajibikaji na uadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya TEMESA jijini Dodoma, Kilahala amesema kuwa Taasisi hiyo inategemea nguvu kazi mpya iliyoingia ili kuendeleza juhudi za maboresho na utoaji wa huduma bora kwa Umma.

“Ni muhimu mkatambua kuwa mmeingia kazini katika kipindi ambacho TEMESA inatekeleza mikakati ya mabadiliko makubwa ya kiutendaji hivyo mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata maadili ya kazi, kuwa wawazi na kujituma kwa ajili ya maendeleo ya Taasisi na Taifa,” amesema Kilahala.

Ameongeza kuwa mwenendo na tabia za watumishi kazini vina mchango mkubwa katika taswira ya Taasisi mbele ya wateja na wadau wake. Hivyo, aliwataka watumishi hao wapya kujiepusha na vitendo visivyoendana na maadili ya utumishi wa umma.

Mafunzo hayo yatachukua siku tatu na yanahusisha watumishi wapya waliopangiwa vituo mbalimbali vya kazi ndani ya TEMESA na yanatarajiwa kuwajengea uwezo katika maeneo ya maadili, sheria za utumishi wa Umma, utendaji bora na utoaji wa huduma kwa wateja.