​“TUITENGENEZE TAASISI YETU TUWE MFANO WA KUIGWA KWENYE HII SEKTA,”KAIMU MTENDAJI MKUU TEMESA

News Image

Posted On: December 15, 2025

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Moses R. Mabamba amewataka mameneja wa Mikoa na vituo vya Wakala huo kufanya kazi kwa bidii ili kubadilisha mitazamo ya watumishi na wanaopewa huduma na Wakala ili kuufanya kuwa mfano wa kuigwa na Taasisi zingine za Umma.

Mabamba ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na mameneja wa Mikoa na vituo Tarehe 13 Disemba, 2025 katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wakala mjini Dodoma ambapo amewaagiza mameneja hao kufanya kazi kwa bidii ili kutoa huduma bora kwa Serikali na jamii kwa ujumla ambazo zitaifanya TEMESA iweze kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maslahi bora ya watumishi.

“Tufanye kazi tuzalishe, tulete hela tuwalipe watumishi, mfanyakazi ni rasilimali ya thamani kwenye Taasisi na ndiye ambaye anaifanya biashara yako ifanyike, tunahitaji kujenga taswira yetu nzuri ili kuwapa imani wateja wetu.” Ameongeza Mabamba.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mtendaji Mkuu amewapa miezi mitatu watumishi wazembe ambao hawataki kufanya kazi kubadilika na amewapa miezi mitatu kuanzia sasa watumishi hao kubadilika ama la sivyo watafikiwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

“Lakini wale walioshindikana kabisa mtanipa na mimi huwa sio muumini wa watu ambao hawataki kufanya kazi, ukiuliza mtu yoyote upande wangu mbaya huwa ni huo na napenda kuutekeleza kwa haraka sana, kwa hiyo wale watoboa mitumbwi tuwape muda kwanza wajibadilishe, tuwape miezi mitatu.’’ Amesema Mabamba.

Aidha, Mabamba amewaagiza mameneja hao kufikiria kibiashara kwakuwa maeneo mengi ya Wakala huo yanashawishi kufanyika kwa biashara kutoka vyanzo vingine na kuongeza kuwa faida kubwa ambayo TEMESA inayo ni kuwa na maeneo maeneo ya thamani yenye kushawishi ufanyikaji wa biashara.