WAZIRI ULEGA AWATAKA WAKANDARASI KUONGEZA KASI YA UJENZI WA KIVUKO KIPYA MAFIA–NYAMISATI

News Image

Posted On: December 08, 2025

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia–Nyamisati kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha anamaliza kazi hiyo kwa viwango vya juu na ndani ya muda uliopangwa.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko hicho katika kata ya Kimbiji, wilayani Kigamboni, Waziri Ulega amesisitiza kuwa mradi huo ni wa kimkakati kwa ustawi wa wananchi wa Mafia Mkoani Pwani, hivyo ni muhimu kazi ifanyike kwa kasi na weledi.

“Nasisitiza mkandarasi afanye kazi usiku na mchana. Ongezeni vijana zaidi kwenye kazi hizi, kwani tuna vijana wengi wa Kitanzania wanaotafuta fursa za ajira. Lengo ni kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili,” alisema Waziri Ulega.

Aidha, ameelekeza kuwa watumishi wote waliopata nafasi ya kushiriki katika mradi huu wapewe vyeti vya kutambua ushiriki wao, ili kuwajengea uwezo na kuwaandaa kushiriki katika miradi mingine ya kitaifa siku zijazo.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bw. Moses Rajab Mabamba, amesema kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko hicho kipya.

Bw. Mabamba alibainisha kuwa hadi sasa mradi umefikia asilimia 57 ya utekelezaji na kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za usafiri kati ya Mafia na Nyamisati, na pia kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Mbunge wa Kigamboni, Sanga Nyakisa, ameomba wizara kutatua changamoto za vivuko vya MV KIGAMBONI na MV MAGOGONI, akisema vimekuwa vikiwasababishia wananchi wa Kigamboni kero kubwa ya usafiri.