WATAALAMU NA WASIMAMIZI WA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI YA TIKETI ZA VIVUKO TEMESA WAPATIWA MAFUNZO

News Image

Posted On: March 27, 2018

Kampuni ya Maxcom Africa Limited imeanza kutoa mafunzo kwa wataalamu wa TEHAMA na wasimamizi wa mifumo ya kielektroniki ya kukatia tiketi katika vivuko vya Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA. Mafunzo hayo ambayo yatachukua wiki mbili yanaratibiwa na kampuni ya Maxcom Africa Limited na yana lengo la kuhakikisha kwamba wataalamu hao wanajengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo mara kwa mara zimekuwa zikijitokeza katika mifumo hiyo ya kielektroniki ya kukatia tiketi katika vivuko vya wakala.

Itakumbukwa kuwa TEMESA kwa sasa imeanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika vivuko vyake vyote nchini na kwa kuanzia mifumo hiyo ilianza kutumika katika vivuko vya Kigongo na Busisi mkoani Mwanza na Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mifumo hiyo ya kielektroniki ya kukatia tiketi imewekwa kuhakikisha kuwa mapato ya wakala yanakuwa wazi na kuepuka udanganyifu na pia kuweka rekodi sawa ya abiria amabao wanatumia vivuko vya wakala lakini pia kudhibiti mapato ya serikali yanayotokana na huduma za vivuko kote nchini.

Mtaalamu wa TEHAMA kutoka wakala huo Victor Rweyemamu amesema mafunzo hayo yanayolenga kuleta ufanisi katika kazi yatarahisisha kazi yao kwa kiasi kikubwa kwani hawatahitaji tena wataalamu kutoka Maxcom mara mashine hizo zitakapopata hitilafu kama ambavyo ilikua hapo awali ambapo ilikua ikiwabidi kusubiria wataalamu kutoka kampuni hiyo kuja kurekebisha tatizo.

Mafunzo hayo yaliyoanza Tarehe 19/03/2018 yanatarajiwa kumalizika Machi 30 mwaka huu.