VIVUKO TEMESA VYAJIIMARISHA KUZUIA CORONA

News Image

Posted On: April 08, 2020

Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kupitia Vivuko vyake vyote nchini imeendelea kujidhatiti kwa kuhakikisha hakuna ongezeko la maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Vivuko vyote vimeendelea kuhakikisha vinatoa elimu kwa watumishi wa Vivuko pamoja na abiria wanaotumia Vivuko hivyo kwa kufuata kanuni na taratibu za afya kwa ajili ya kujikinga na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi hivyo.

“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika vivuko vyetu vyote kuanzisha utaratibu wa abiria kunawa kabla na baada ya kuingia kwenye Vivuko kwa sababu watu wanatuelewa na wanaipokea elimu juu ya kujikinga na kuchukua tahadhari,”alisem Meneja wa TEMESA mkoa wa Mwanza Mhandisi Karonda.

Kwa kushirikiana na wataalamu wa afya kutoka Health Port vituoni hapo wamekuwa wakiendesha zoezi la kuwapima joto la mwili kwa kifaa maalumu cha kupimia joto abiria wanaotumia Vivuko hivyo na kuwasisitiza kunawa mikono kwa maji yaliyochanganywa na dawa aina ya chlorine kwa ajili ya kujikinga na maambukizi.

Vivuko hivyo vimefanikiwa kununua vifaa mbalimbali vya kujikinga na maambukizi ya Covid-19 kwa ajili ya watumishi wanapokuwa wanatoa huduma kwa abiria. Vifaa hivyo ni barakoa (mask), glovu pamoja na vitakasa mikono (saniters).

Aidha kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19 nchini Wakala kupitia Vivuko unaendelea kutoa elimu ya tahadhari na kujikinga na maambukizi ya virusi hivi kwa kuendelea kutoa elimu na taarifa muhimu kupitia “Social Media” za Wakala kuelezea njia za kutumia kujikinga ili kuzuia virusi hivi vya Corona visiendelee kusambaa nchini.