MATUMIZI YA MFUMO UFUATILIAJI NA TATHMINI, CHACHU YA MAENDELEO TEMESA

News Image

Posted On: August 27, 2024

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala amewataka washiriki wanaopata Mafunzo ya matumizi ya mfumo wa ufuatiliaji wa tathmini kuwa walimu wa watumishi wengine ili waweze kuchochea namna sahihi ya ufanyaji kazi bila kusua sua katika majukumu yao.

Mtendaji Mkuu ameyazungumza hayo Agosti 26, wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa ufuatiliaji wa tathmini yaliyoratibiwa na Wizara ya Ujenzi. Mafunzo hayo yafanyika katika ukumbi wa mikutano wa TEMESA Makao Makuu mjini Dodoma.

Kilahala amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati sahihi ambapo yatajenga uwezo wa kujua kinachoendelea kwenye mfumo wa ufuatiliaji na kutatua changamoto za mkanganyiko wa taarifa kwenye vitengo tofauti.

“Kikubwa hapa mfumo huu utatusaidia kuwa na taarifa sahihi kwa wakati sahihi ili wa sera atengeneze sera, wa maamuzi ya uendeshaji afanye maamuzi lakini hata wewe meneja pale kwako unajua nini kinachoendelea” amesema Mtendaji Mkuu.

“Kumekuwa na changamoto unaweza ukaleta taarifa moja katika lengo lile lile kwa siku tofauti ukapata taarifa tofauti tofauti kwahiyo inaleta mkanganyiko kwenye upande wa sera, eneo la uendeshaji na kwa kila mtu hivyo huu mfumo utakwenda kutuondolea hili tatizo” Alisisitiza Kilahala.

Aidha Mtendaji Mkuu amesisitizia kuwa mafunzo hayo ni chachu ya mabadiliko ya nguvu ya utendaji kazi utakaopelekea TEMESA kuwa mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku tano yamehudhuriwa na muwakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, Mameneja na watumishi kutoka Mikoa yote na vituo vya TEMESA Nchini.