UJENZI WA VIVUKO VIPYA VITATU KUKAMILIKA MWEZI AGOSTI 2020

News Image

Posted On: July 20, 2020

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA inatarajiwa kukamilisha ujenzi wa vivuko vipya vitatu ifikapo mwezi Agosti mwaka huu. Hayo yamebainishwa leo wakati Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala huo Profesa Idrissa Mshoro alipotembelea kujionea ujenzi wa vivuko viwilli kati ya vitatu vinavyoendelea kujengwa katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela mkoani Mwanza. Akiwa katika ziara hiyo, Profesa Mshoro pia alipata wasaa wa kukagua ukarabati unaoendelea kufanyika katika karakana ya mkoa iliyopo maeneo ya Igogo jijini Mwanza.

Akizungumza katika ziara hiyo Profesa Mshoro alisema ujenzi wa vivuko hivyo ulipaswa kuwa umekamilika mapema mwaka huu lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Covid19 kulisababisha kufungwa kwa mipaka na hivyo kuzuia uingizwaji wa vifaa kutoka nchi ambazo zilikua zimeathirika na ugonjwa huo.

“Ukamilikaji wa vivuko hivi, kile cha Kayenze Bezi ambacho taayri kinatoa huduma, Bugorola Ukara, Chato Nkome na cha Mafia Nyamisati vitatoa ahueni kubwa sana kwawananchi wa maeneo hayo husika”, alisema Profesa Mshoro ambapo pia aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuendelea kutoa fedha ambazo zinawezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo vivuko na uboreshaji wa karakana.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mtakwimu Bi Suzan Ndunguru aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwapa kipaumbele wakazi wa Mwanza kwa kuendelea kuwasogezea kwa karibu huduma ya usafiri wa majini.

Halikadhalika, Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Major Songoro alibainisha kuwa uwekaji wa injini tayari umekwishakamilika katika vivuko hivyo na hivyo mpaka kufikia mwezi wa nane vivuko vyote vitakua tayari kuingizwa majini kwa ajili ya ukaguzi ili kuweza kuanza kazi mara moja. Alitumia fursa hiyo pia kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuziamini kampuni za wazalendo ikiwemo kampuni ya Songoro na kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi kwa ujumla.

Awali, wakiwa kwenye karakana ya mkoa wa Mwanza, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma taarifa kuhusu ukarabati wa karakana alisema Wakala umeanza kukarabati kwa awamu karakana zake ili kubadili muonekano na kuondoa uchakavu ambapo amezitaja karakana hizo kuwa ni karakana ya mkoa wa Mwanza ambayo ukarabati wake unaendelea na unafanywa na vikosi vya ujenzi tawi la Mwanza, karakana ya mkoa wa Mbeya ambayo inafanywa na mkandarasi vikosi vya ujenzi tawi la Dar es Salaam, karakana ya Dodoma, karakana ya Dar es Salaam, karakana ya MT. Depot pamoja na karakana ya mkoa wa Singida.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha yote iliyokuwa imepangwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2019/ 2020 shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa karakana”, alisema Mtendaji Mkuu. Aliongeza kuwa Wakala umeanzisha karakana ngazi ya Wilaya katika Wilaya ya Same, Halmashauri ya mji waIfakara (Kilombero) mkoani Morogoro pamoja na Kahama Shinyanga. Vilevile karakana ngazi ya Wilaya zinatarajiwa kuongezwa pia katika Wilaya za Simanjiro na Masasi.

Aidha kwa upande wa vivuko Mhandisi Maselle alibainisha kuwa mpaka kufikia Disemba mwaka 2019 serikali ilikuwa imetoa shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ununuzi wa vivuko vipya, maegesho na miundombinu ya vivuko.

“ Kivuko cha Bugorola Ukara kimefikia asilimia 80% ambapo kikikamilika kitagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.2, kivuko cha Chato – Nkome kitagharimu shilingi bilioni 3.1 nacho kimefikia aslimia 80%, kivuko cha Kayenze- Bezi kimekamilka na kilianza kazi kuanzia mwezi Mei 2020 na kimegharimu shilingi bilioni 2.7, kivuko cha Mafia -Nyamisati kimefikia asilimia 70% na kinagharimu shilingi bilioni 5.3” alisema Mtendaji Mkuu.

Mhandisi Maselle alimaliza kwa kusema kuwa vivuko hivyo sasa vinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu baada ya mkandarasi M/S Songoro Marine Transport Ltd wa Mwanza kuongezewa muda wa ujenzi wa vivuko hivyo kutokana na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu Covid19 ambalo lilisababisha kusimama kwa ujenzi kutokana na ucheleweshwaji wa vifaa kutoka nje ya nchi.