WAKAZI ZAIDI YA 15,000 KUNUFAIKA NA HUDUMA YA USAFIRI WA KIVUKO KATA YA KANYALA HALMASHAURI YA MJI BUCHOSA WILAYANI SENGEREMA MKOANI MWANZA
Posted On: July 15, 2025
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) inatarajia kupeleka huduma ya kivuko katika Kata ya Kanyala Halmashauri ya Mji Buchosa Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ili kutatua changamoto ya usafiri inayowakabili wakazi wa kata hiyo na Kata ya Soswa.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala amesema hayo leo alipokuwa akikagua eneo ambalo yatajengwa maegesho ya kivuko pamoja na miundombinu yake ikiwemo majengo ya kupumzikia abiria na ofisi kwa ajili ya kutoa huduma katika eneo hilo.
Kilahala amesema, Kivuko cha MV. SENGEREMA ambacho hapo awali kilikuwa kinatoa huduma kati ya Kigongo na Busisi, kinatarajiwa kupelekwa eneo hilo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma na kwa kuanza kitakuwa kikitoa huduma kati ya eneo la Kanyala na Kasarazi.
‘’Hawa wananchi wa maeneo haya kama tunavyoona shughuli zao kubwa ni za uvuvi na wanafanya pia shughuli nyingine za kiuchumi kwahiyo uwepo wa kivuko kikubwa cha uhakika kwakweli itakuwa ni msaada mkubwa kwenye shughuli zao za kiuchumi na ni imani yetu kabisa kwamba hili jambo litafanyika kwa wakati kama nilivosema, lakini pia wananchi nao waendelee kuona matunda ya kuwa na Serikali sikivu ambayo inatatua changamoto zao kadiri zinavyoifikia’’. Amesema Kilahala.
Katika Kata hizo mbili, kuna vitongoji takribani saba na hakukuwahi kuwepo na huduma yoyote ya kivuko zaidi ya uwepo wa boti ndogo za mbao ambazo ni ghali na si salama sana kwa matumizi kwa wakazi hao hivyo kupelekwa kwa kivuko cha MV. SENGEREMA katika eneo hilo kutachochea shughuli za kibiashara na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa Kata hizo na majirani zao kwa kiasi kikubwa.