TEMESA YAANZA KAMPENI YA MLANGO KWA MLANGO KUKAGUA MAGARI YA TAASISI ZA SERIKALI
Posted On: July 07, 2025
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kupitia ofisi yake ya Mkoa wa Dar es Salaam, imezindua rasmi kampeni ya Mlango kwa Mlango (Door to Door) yenye lengo la kuzifikia Taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kutoa huduma ya ukaguzi wa magari moja kwa moja katika maeneo yao ya kazi.
Kampeni hii imelenga kuhakikisha kuwa magari ya Serikali yanakuwa katika hali bora ya kiusalama na kiufundi, yanatunzwa kitaalamu, na yanadumu kwa muda mrefu kwa kufuata miongozo ya kitaaluma. Aidha, huduma hiyo inahusisha pia usajili wa magari katika Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM), ambao unaziwezesha Taasisi kujua hali halisi ya magari yao na kupanga bajeti ya matengenezo kwa usahihi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Meneja wa TEMESA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Liberatus Bikulamchi amesema kampeni hiyo inalenga kusaidia Taasisi za Serikali kupata tathmini sahihi ya hali ya magari yao, jambo litakalowasaidia kupanga bajeti ya matengenezo kwa ufanisi huku wakijenga utamaduni wa kufanya matengenezo kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu za kiufundi.
"Kupitia kampeni hii, tunaleta huduma moja kwa moja kwa wateja wetu ili kuwasaidia kuwa na taarifa sahihi kuhusu magari yao, kufanya maamuzi sahihi ya matengenezo na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za Umma," alisema Mhandisi Bikulamchi.
Aliongeza kuwa mfumo wa kidigitali wa MUM ni nyenzo muhimu itakayosaidia Taasisi kufuatilia historia ya matengenezo ya kila gari, hivyo kusaidia kupanga bajeti kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Leonard Bruno Tumua, ameishukuru TEMESA kwa kutoa huduma hiyo ya ukaguzi kwa magari ya Taasisi pamoja na magari ya watumishi wa TCAA.
"Huduma tumeiona kuwa ni nzuri sana. Magari yote ya Taasisi yamekaguliwa na kwa yale yaliyoonyesha changamoto, tumepata ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuzitatua na kuyafanyia matengenezo," alieleza Bw. Tumua.
TEMESA Dar es Salaam inaziomba Taasisi za Serikali kuiunga mkono na kushiriki kikamilifu katika kampeni hii kwa kushirikiana na timu za wataalamu zitakazotembelea maeneo yao.