TEMESA YAWEKA KAMBI MAONESHO YA 49 YA BIASHARA YA KIMATAIFA SABASABA
Posted On: July 04, 2025
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unashiriki kikamilifu katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kutoa elimu kwa umma juu ya huduma zake na mikakati ya mabadiliko inayoendelea ndani ya taasisi hiyo.
Kupitia banda lake lililopo kwenye maonesho hayo, TEMESA inatoa maelezo ya kina kuhusu huduma mbalimbali inazotoa, ikiwemo matengenezo ya magari ya serikali, huduma za vivuko, ushauri wa kihandisi, ukodishaji wa mitambo pamoja na mfumo mpya wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) unaolenga kuongeza uwazi, ufanisi na utunzaji sahihi wa kumbukumbu.
Aidha, TEMESA inatumia fursa hiyo kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi kwa njia ya ubia (PPP) kwenye uwekezaji wa vivuko, mitambo na karakana mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo kujitegemea kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali wametembelea banda la TEMESA na kupata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu namna ya kushirikiana na taasisi hiyo katika kutoa huduma bora zaidi kwa taifa.
TEMESA inawakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, ili kupata elimu kuhusu huduma zetu, kujionea teknolojia na mifumo tunayotumia, pamoja na kujadiliana fursa mbalimbali za ushirikiano.
Karibu ujifunze zaidi kuhusu mwelekeo mpya wa TEMESA katika kuboresha huduma na kuleta tija kwa Taifa!