UJENZI WA KIVUKO KIPYA KAYENZE BEZI WAANZA RASMI

News Image

Posted On: March 13, 2019

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA imefanikisha kuanza rasmi kwa ujenzi wa kivuko kipya kitakachotoa huduma kati ya Kayenze na Bezi Wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Zoezi la uwekaji msingi wa kivuko (Keel Laying) limefanyika katika yadi ya Songoro iliyopo katika eneo la Pasiansi ambalo hutumiwa kwa ajili ya ujenzi wa vivuko. Ujenzi wa kivuko hicho ambao unatarajiwa kuchukua miezi kumi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 na unafanywa na kampuni ya kizalendo ya ‘’Songoro Marine Transport Boatyard’’ ya jijini Mwanza

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle ameitaka kampuni iliyoshinda Zabuni ya ujenzi wa kivuko hicho ambayo ni Songoro Marine Transort ya Mwanza, kuifanya kazi hiyo kwa uharaka, ubora na pia kuimaliza kwa wakati ili wakazi wa maeneo hayo waweze kupata kivuko hicho mapema na kufaidika na uboreshaji wa huduma ya usafiri unaofanywa na serikali kisiwani humo.

Aidha, Mhandisi Maselle amesisitiza kuwa mkataba kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya cha Bugorola kwenda Ukara unategemewa kusainiwa mapema wiki hii na ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo kama hiyo ambayo inaboresha huduma za usafiri kwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoroo Salehe Songoro, ameahidi kuukamilisha mradi huo katika muda uliopangwa na akaishukuru serikali kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa zabuni ya ujenzi wa kivuko hicho.

Kivuko hicho kitawawezesha wakazi wa maeneo hayo kusafirisha bidhaa mbalimbali kwenda kisiwani humo, kuvusha wanafunzi wa shule pamoja na kusaidia huduma za afya kupatikana kwa wepesi na kitakapokamilika kitakua na uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 kwa wakati mmoja sawa na tani 85 na kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa wakazi wa maeneo hayo.