TEMESA imeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kuunga mkono ubunifu na maendeleo ya vijana katika mashindano ya andiko la ubunifu kuhusu namna ya kupunguza msongamano wa magari mijini, yanayofahamika kama Wanafunzi Challenge 2026.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa zawadi iliyofanyika tarehe 10 Mei, katika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameishukuru TEMESA kwa kuunga mkono jitihada hizo zinazolenga kuhamasisha matumizi ya maarifa, ubunifu na nguvu za wanafunzi katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo nchini.
Waziri Ulega amesema lengo la mashindano hayo ni kuhakikisha wanafunzi wanatumia elimu ya nadharia kwa vitendo kupitia mawazo bunifu yatakayosaidia kuboresha mifumo ya usafiri na kupunguza msongamano wa magari mijini, hali itakayochochea maendeleo ya taifa.
“Ni muhimu kuendelea kuwashirikisha vijana kikamilifu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa kupitia elimu, teknolojia na ubunifu,” amesema Waziri Ulega.
Katika mashindano hayo, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bw. Tukay David Thomas, ameibuka mshindi wa kwanza baada ya kuonesha ubunifu mkubwa katika kuwasilisha mawazo ya kupunguza changamoto za usafiri mijini. Kutokana na ushindi huo, amejishindia hundi ya shilingi milioni 10, ngao, kompyuta mpakato pamoja na cheti.