TEMESA YANG'ARA MAADHIMISHO YA KITAIFA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA DODOMA

News Image

Posted On: June 20, 2026

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeshiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni, 2026 katika viwanja vya Chinangali, Mkoa wa Dodoma. Maadhimisho hayo yalilenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kusikiliza na kutatua changamoto za kiutumishi pamoja na kuimarisha uwajibikaji na utawala bora katika utoaji wa huduma za umma.

Katika kipindi chote cha maonesho hayo, wananchi wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma walitembelea banda la TEMESA kupata elimu kuhusu huduma na majukumu ya wakala huo. Wananchi walipata fursa ya kufahamu kwa undani huduma za matengenezo ya magari na mitambo, kazi za umeme, TEHAMA na elektroniki, pamoja na miradi ya ujenzi na ukarabati wa vivuko inayotekelezwa na TEMESA katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa wageni waliotembelea banda la TEMESA alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Arusha, Bw. Suleyman Msumi, ambaye aliipongeza TEMESA kwa hatua ya kuanzisha mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa huduma za matengenezo. Alieleza kuwa mifumo hiyo imerahisisha mchakato wa kuomba huduma za magari, umeme na elektroniki kwa kupunguza muda wa kusubiri na kuondoa urasimu.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Bw. Msumi alisema:"Wote mnafahamu TEMESA ni shirika la Serikali na sisi taasisi za Serikali, nikizungumzia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa namaanisha Halmashauri pamoja na Serikali Kuu, ni wadau wa TEMESA hususan katika kutengeneza magari, mitambo na vifaa vingine. TEMESA imefanya maboresho makubwa sana katika miundombinu yake na katika utoaji wa huduma. Kuna mashine nyingi sana za kisasa, na mimi ni shuhuda kwa sababu nikiwa kama msimamizi namba moja wa Halmashauri nalithibitisha hilo."

Aidha, alieleza kuwa Halmashauri ya Mji wa Arusha imeendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na TEMESA na kuwataka viongozi wa taasisi nyingine za Serikali kuendelea kutumia huduma hizo kutokana na ubora wake."Sisi ni wadau wa TEMESA na magari yetu, huduma za matengenezo kinga zote, ukarabati wote na kila kitu tunapeleka TEMESA. Ninawasihi viongozi wengine wa taasisi za Serikali kutumia huduma za TEMESA kwa ubora zaidi, thamani halisi ya fedha na uhakika wa vipuri vinavyofungwa kwenye magari. Kwa sasa TEMESA imeboreshwa sana, ina mafundi wabobezi na wanafanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu."

Mbali na pongezi hizo, Bw. Msumi alishauri wataalamu wanaosimamia magari na mitambo mikubwa kuendelea kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ufanisi, weledi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wateja.

Maonesho hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yalifunguliwa rasmi tarehe 17 Juni, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete. Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, TEMESA imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa, kuimarisha ufanisi wa shughuli zake na kujenga mahusiano bora na wananchi pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali.