​PROFESA RIZIKI SHEMDOE ATEMBELEA BANDA LA TEMESA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA, AIPONGEZA KWA MCHANGO MKUBWA WA MAENDELEO

News Image

Posted On: June 24, 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, tarehe 23 Juni, 2026 ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa akiwa bandani hapo, Profesa Shemdoe ameipongeza TEMESA kwa kupata muundo mpya wa utendaji kazi, akisema hatua hiyo itaiwezesha taasisi hiyo kuendelea kupiga hatua zaidi huku ikiwajengea watumishi ari ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, weledi na kujituma.

Aidha, amesema Serikali imeikabidhi TEMESA majukumu mbalimbali ya msingi yenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taifa, hivyo akaitaka taasisi hiyo kuendelea kuyatekeleza kwa ufanisi na kuwajibika ipasavyo.

Profesa Shemdoe pia ameipongeza TEMESA kwa kutimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake tarehe 23 Juni, 2006, akieleza kuridhishwa na mchango wa wakala huo katika kutoa huduma bora kwa Watanzania.

“Nina furaha kubwa kufika katika banda lenu la TEMESA mkiwa mnatimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwenu. Kazi nzuri mnayoifanya iendelee, na yale yenye mapungufu yaendelee kufanyiwa kazi ili tuendelee kusonga mbele katika kulitumikia taifa letu na Watanzania kwa ujumla. Natamani ifikapo mwaka 2050, TEMESA iwe taasisi bora zaidi,” amesema Profesa Shemdoe.

Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yalidumu kwa muda wa wiki moja kuanzia Juni 16, 2026, na yamefungwa rasmi na Profesa Riziki Shemdoe.