MAAFISA USAFIRISHAJI WATAKIWA KUSIMAMIA UTUNZWAJI WA MALI ZA SERIKALI
Posted On: September 29, 2023
Maafisa usafirishaji wa Taasisi za Umma wametakiwa kusimamia nyezo za kusaidia utendaji kazi Serikalini ili kuimarisha ufanisi na utendaji kazi na utunzwaji wa mali za Umma.
Hayo yamebainishwa leo Tarehe 29 Septemba 2023 na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar Bw. Shomar Omar Shomar wakati wa Kikao cha wadau wanaotumia huduma za Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kilichofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Visiwani humo huku kikao hicho kikiwalenga maafisa Usafirishaji ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanaosimamia magari yote ya Serikali katika Taasisi zao.
Katibu Mkuu amewataka maaafisa Usafirishaji kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanasimamia vizuri masuala ya usafiri na huduma za ufundi. ‘’Hivi sasa Serikali ipo katika utaratibu wa kuandaa muongozo wa matumizi mazuri ya gari za Serikali lakini Serikali imekuwa ikifuatiliakwa karibu sana matumizi ya magari hayo, kila Katibu Mkuu na Mtendaji Mkuu ana wajibu wa kuhakikisha gari zilizokuwa chini yaTaasisi yake anazisimamia vizuri.’’ Amesema Katibu Mkuu ambapo pia amegusia masuala mazima ya nyenzo za utendaji kazi ambazo ni mpango mkuu wa Taifa unaohusiana na masuala ya usafirishaji hasa ufundi na matengenezo ya magari.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda, akizungumza katika kikao hicho amehimiza ushirikiano na utunzaji wa mali za Serikali huku akisisitiza kuwa kikao hicho kinalenga kuwafundisha maafisa usafirishaji hao namna bora ya utunzaji wa magari ya Serikali ili yaweze kuleta tija katika kuhudumia wananchi kwa gharama nafuu kwa watumiaji na hata kwa Serikali.
‘’Leo tutapata semina maalumu kwasababu kuna malengo ambayo tunataka myapate ya namna bora ya utunzaji magari ya Serikali ili yaweze kuleta tija kuhudumia wananchi na kwa gharama nafuu kwa watumiaji na hata kwa Serikali. Amesema Mhandisi Karonda.
Meneja wa TEMESA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Liberatus Bikulamchi akizungumza katika mafunzohayo amesema programu hiyo ikikamilika anaamini maafisa hao watakuwa na uelewa wa pamoja wa jinsi ya kusimamia utunzaji mzuri wa magari pamoja na uelewa wa pamoja wa vitu gani vya msingi vya kufanyia matengenezo katika magari.