MAAFISA USAFIRISHAJI, GEREJI TEULE KAGERA WAPATIWA MAFUNZO MFUMO WA KIDIGITALI WA TEMESA MUM
Posted On: April 26, 2025
Maafisa usafirishaji pamoja na wasimamizi wa Gereji Teule zinazofanya kazi kwa pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoani Kagera wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuutumia Mfumo wa kidigitali wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo unaojulikana kama (MUM) ikiwa ni kampeni endelevu ya mabadiliko makubwa yanayoendelea katika TEMESA.
Mafunzo hayo, yameongozwa na Meneja wa TEMESA Kikosi cha Umeme Mhandisi Pongeza Semakuwa, na yamefanyika katika ukumbi wa St.Therese ulioko Mkoani Kagera na yamelenga kuwafundisha maafisa hao kutoka Taasisi za Seikali na Gereji Teule kuhusu matumizi sahihi ya mfumo huo wa kidigitali, ambao umeanzishwa ili kuongeza ufanisi, uwazi, na uwajibikaji katika usimamizi wa kazi za mafengenezo ya magari, mitambo, makangavuke, lifti, viyoyozi, kazi za mifumo ya TEHAMA na elektroniki pamoja na kazi za kusimika mifumo ya umeme katika majengo ya Serikali.
Akizungumza wakati akiendesha mafunzo hayo Mhandisi Semakuwa amesisitiza umuhimu wa mfumo wa MUM kwa Taasisi za serikali na kuwasihi maafisa hao kuutumia kiusahihi kwa faida ya taasisi zao za Serikali, binafsi na taifa zima kwa ujumla.
"Mfumo huu ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa uwazi na kwa wakati, sambamba na kuimarisha usimamizi wa mali za umma."alisema mhandisi Pongeza.
Washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Meneja wa mkoa wa Kagera Mhandisi Prisca ameelezea kufurahishwa na elimu waliyopatiwa washitiri wake, huku akiahidi kutumia maarifa hayo katika kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.
TEMESA inaendelea na kampeni ya mafunzo ya mfumo wa kidigitali wa MUM nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kutumia TEHAMA kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.