MAFUNZO YA MFUMO WA USIMAMIZI WA HUDUMA ZA MATENGENEZO KUBORESHA HUDUMA TEMESA

News Image

Posted On: March 04, 2025

Menejimenti na baadhi ya Watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) leo wamekutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Wakala huo, makao makuu jijini Dodoma na kufanya kikao cha mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM).

Kikao hicho cha mafunzo kilichoongozwa na Mtendaji Mkuu Lazaro Kilahala kimelenga kuimarisha ufanisi wa usimamizi wa kazi za matengenezo na kuhakikisha kuwa mifumo ya kiteknolojia inatumika vyema ili kuboresha huduma za kiufundi na umeme zinazotolewa na TEMESA.

Katika mafunzo haya, watumishi wamefundishwa namna sahihi ya kutumia mfumo kwa ufanisi zaidi, pamoja na faida za mfumo huo katika kuboresha ubora wa huduma, kupunguza ucheleweshaji na kuongeza uwazi katika utendaji wa kazi za matengenezo.

Mtendaji Mkuu pia amesisitiza umuhimu wa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.