TOTAL ENERGIES YATOA MAFUNZO KWA MAFUNDI TEMESA
Posted On: August 22, 2023
Kampuni ya kimataifa ya Vilainishi Total Energies Tawi la Dar es Salaam Tanzania, leo imetoa mafunzo ya matengenezo ya magari upande wa vilainishi kwa mafundi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), mafundi kutoka karakana teule pamoja na wauzaji wa vipuri na vilainishi vya matengenezo ya magari.Mafunzo hayo ya siku moja, yametolewa mjini Dodoma katika hoteli ya Best Western Dodoma Hotel na mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Tanzania (NIT) akishirikiana na mkufunzi kutoka kampuni hiyo huku yakishirikisha mafundi kutoka Mikoa ya Dodoma, Tabora, Singida pamoja na Iringa.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda amesema Wakala huo kwa kushirikiana na Total Energies wameandaa mafunzo hayo kwa mafundi ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi hasa wakati wanapotumia vilainishi. Mhandisi Karonda amesema vilainishi ni mojawapo ya kitu muhimu sana wakati wa matengenezo ya magari, hivyo TEMESA imetumia nafasi hiyo kuwapa mafundi hao mafunzo kutoka karakana za Wakala pamoja na karakana Teule ambazo zinafanya kazoo pamoja na Wakala, lengo kuu likiwa ni kuhudumia vizuri magari ya Serikali.
‘’Total tunao mkataba nao, ndio wazabuni wetu katika kusambaza vilainishi katika karakana zetu, kwahiyo tumeanza nao hawa lakini tunawakaribisha wazabuni wengine kama ORYX, nao tunaweza kufanya nao mafunzo kama haya, lengo likiwa ni kuelimisha mafundi wetu na kuweza kutoa huduma nzuri.’’ Amesema mhandisi Karonda ambapo ameongeza kuwa mafunzo hayo ya siku moja yameanzia Mkoani Morogoro na kufuatia Mkoani Dodoma, lakini pia yatatolewa Mkoani Mwanza, Kagera (Bukoba), Arusha, Mbeya, Ruvuma (Songea) pamoja na Mtwara.
Aidha, Mkurugenzi amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni endelevu kwa mafundi na kwa upande wa Kanda ya Ziwa mafunzo hayo yatashirikisha Mikoa ya Kanda hiyo ambapo mafunzo hayo yatatolewa siku ya Tarehe 23 Agosti, yakishirikisha pia mafundi upande wa vivuko.
‘’Vilainishi vinatumika hata kwenye vivuko na mitambo mbalimbali kwahiyo ni mafunzo muhimu sana kuwapatia wataalamu wetu.’’ Amesisitiza Mhandisi Karonda huku akitoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi inazoendelea kuzifanya ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta binafsi na kuboresha mazingira ya Sekta ya Umma ili kuweza kushirikiana na kampuni binafsi katika kuboresha utoaji huduma ikiwemo mafunzo kwa watumishi wa karakana pamoja na watumishi wa karakana binafsi teule ambao wanafanya kazi pamoja na TEMESA.
Naye Mhandiri kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Michael Kyando, akizungumza mara baada ya kutoa mafunzo hayo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuangalia hasa namna ya kulinda vyombo vya usafiri hasa magari, pikipiki, mitambo na magari makubwa ambayo yanafanyiwa matengenezo katika karakana za Wakala pamoja na karakana binafsi Teule. ‘’Kama tunavyofahamu kwamba vilainishi ndiyo maisha ya injini, kwahiyo watu wa Total Energies wanasambaza hivi vilainishi, wameamua sasa kufanya mafunzo ili kusudi hawa watumiaji wa hivi vilainishi waweze kutumia vile vilainishi ambavyo vinatakiwa kulingana na mtengenezaji alivoelekeza lakini pia kulingana na mazingira ambayo tunaishi nayo, kwahiyo mimi kama mtaalamu nimeona ni mafunzo ambayo kwakweli yatasaidia sana kwenye kutunza magari hasa ya Serikali na magari mengine ambayo tunayatengeneza, kwahiyo hawa mafundi wamepata elimu ya kutosha na tunaendelea na hili zoezi kwa karakana zingine kama ilivyoelezwa.’’ Amemaliza Mhandisi Kyando.
Aidha , Meneja wa Mafunzo na Ufundi wa Kampuni ya Total Energies Julius Magele, akizungumzamara baada ya kutoa mafunzo hayo kwa mafundi amesema, wametoa mafunzo hayo hayo kwa jili ya kuwajengea uelewa wa uchaguzi sahihi wa vilainishi pamoja na matumizi yake. ‘’Mafunzo haya ni muhimu kwa mafundi kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kufanya uchaguzi sahihi wa vilainishi na kwakuwa tuko karibu na TEMESA na tunafanya nao biashara sasa hivi ya vilainishi, tumeamua kushirikiana nao kwa ajili hiyo ili waweze kuwa watumiaji wazuri wa vilainishi vyetu napengine mabalozi wazuri na nia pia ni kuendelea kujenga uwezo wa kuwa na utambuzi wa vilainishi na kutofanya makosa kwenye matumizi sahihi ya vilainishi.’’ Amesema Meneja Magele na kuongeza kuwa teknolojia inabadilika kila mara hasa kwenye mitambo mipya ambayo inaingia nchini hivyo kuwepo uchaguzi sahihi wa vilainishi utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwenye mitambo, pamoja na kuiwezesha mitambo hiyo kuweza kudumu kwa muda mrefu.
Nao wanufaika wa mafunzo hayo akiwemo Mhandisi Said Mbwego amesema mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu matumizi sahihi ya kilainishi kwa gari husika ambalo limeingia kwa wakati huo lakini pia wameweza kufahamu ni kilainishi kipi kinafaa kutumika kwa wakati husika. Fundi Sanifu kutoka TEMESA Dodoma Luhende Matinde amesema mafunzo hayo yatamsaidia kujibu baadhi ya maswali ambayo amekuwa akijiuliza kila siku kuhusu aina gani ya kilainishi anaweza kutumia na amesema mafunzo hayo yatamsaidia kumshauri mteja kutumia kilainishi sahihi na ameahidi kuwa balozi mzuri kuelimisha juu ya matumizi ya kilainishi bora na salama.