NAMNA USAFIRI WA MAJINI ULIVYO MWAROBAINI KANDA YA ZIWA
Posted On: October 23, 2025
Tukizungumzia huduma za usafiri na usafirishaji hapa nchini tunaangalia aina mbalimbali za usafiri ambazo hutumiwa na jamii yetu ikiwemo usafiri wa ardhini, angani na usafiri wa maji. Usafiri huu hutegemea mahali husika kutokana na mazingira ya eneo moja na jingine ambapo jamii fulani hulazimika kutumia aina tofauti ya usafiri kwa asilimia kubwa kuliko nyingine. Mathalani kwa upande wa Kanda ya Ziwa, uzoefu unaonyesha kuwa licha ya jamii ya Kanda hiyo kutumia usafiri wa aina mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingina lakini pia hutumia zaidi usafiri wa vivuko.
Kwa kulizingatia hili, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imetekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa vivuko na miundombinu ya maegesho katika maeneo mbalimbali nchini ambapo hadi kufikia Aprili, 2025 Serikali imetekeleza ujenzi na ukarabati wa maegesho ya vivuko na miundombinu katika Mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Geita na Kagera ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kivuko cha Ijinga- Kahangala ambacho kinagharimu kiasi cha shilingi billioni 5.2 na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100, Ujenzi wa kivuko hicho tayari umefikia asilimia 91.
Kivuko cha Bwiro Bukondo (MV. BUKONDO) kinachogharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.5 na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100, Ujenzi wa kivuko hicho tayari umekamilika na tayari kimeshushwa kwenye maji na kinatarajiwa kuanza kufanyiwa majaribio hivi karibuni kabla ya kwenda eneo husika kwa ajili ya kuanza kutoa huduma. Wakati kivuko cha Nyakaliro Kome (MV. KOME III) kinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 8 na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170 huku Ujenzi wa kivuko hicho tayari umefikia asilimia 94.
Halikadhalika, Kivuko cha Buyagu - Mbarika kinagharimu shilingi Bilioni 3.8 ambacho kitatoa huduma katika maeneo ya Buyagu na Mbarika Wilaya za Sengerema na Misungwi Mkoani Mwanza.
Aidha, Kivuko cha Buyagu- Mbarika kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 50 zikijumuisha/abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo (saloon cars) 6. Ujenzi wa kivuko hicho tayari umefikia asilimia 81.
Pia, Kivuko cha Kisorya Rugezi (MV. UKEREWE) kinagharimu Shilingi bilioni 5.5, Kivuko hicho kinao uwezo wa kubeba tani 170, abiria 800 ikijumuisha magari madogo 22. Ujenzi wa kivuko hicho tayari umekamilika, kivuko kimeshushwa kwenye maji na kipo kwenye hatua za mwisho za kumaliziwa kazi ndogo ndogo zilizobakia ikiwemo kupaka rangi kabla ya kufanyiwa majaribio ili kipelekwe eneo la Kisorya na Rugezi kuanza kutoa huduma.
Serikali imeamua kuelekeza vivuko hivi vyote katika Kanda hiyo ili tu kurahisisha huduma za usafiri ambapo inaonekana ni kiungo muhimu kwa jamii za Ukanda huo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme anasemaje kuhusu huduma za usafiri wa vivuko katika kanda hiyo na maeneo mengine nchini.
Mtendaji Mkuu TEMESA, Lazaro Kilahala amesema kuwa Serikali imekamilisha Ujenzi wa maegesho ya kivuko eneo la Kisorya, Bukimwi na upande wa Rugezi ujenzi unaendelea na unakaribia kukamilika ambako kivuko MV. UJENZI kinatoa huduma kikishirikiana na kivuko MV. MISUNGWI ambacho kimeanza kutoa huduma rasmi hivi karibuni baada ya kuhamishiwa eneo hilo kutoka Kigongo- Busisi.
Eneo la Kanyala, Soswa na Kasarazi lililopo Halmashauri ya Mji Buchosa Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza pia Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa miundombinu ya kivuko ambayo ni majengo ya kupumzikia abiria, ofisi pamoja na maegesho ya kivuko. Baada ya ujenzi wa miundombinu hiyo, Serikali inatarajia kupeleka kivuko MV. SENGEREMA kilichohamishwa kutoka eneo la Kigongo- Busisi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma katika eneo hilo.
Eneo la Bwiro na Bukondo, tayari ujenzi wa maegesho kwa pande zote mbili umekamilika kwa asilimia mia moja na kivuko MV. BUKONDO kitakapokamilika kitapelekwa kwa ajili ya kuanza kutoa huduma. Eneo la Kahangala, ujenzi wa maegesho tayari umekamilika na eneo la Ijinga ujenzi bado unaendelea kwa kasi kubwa. Eneo la Buyagu ujenzi wa maegesho tayari umekamilika na eneo la Mbarika ujenzi bado unaendelea na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili.
‘’Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kuimairisha maeneo ya vivuko ili huduma iwe bora zaidi, unaweza kuona ni kwa namna gani Mhe. Rais wetu ambavyo anasikia, anajali na anachukua hatua kwasababu hii yote ni pesa na unajua hii Nchi ina mahitaji mengi ya pesa lakini kwasababu ya mapenzi yake kwa wananchi wa maeneo ya Kanda ya Ziwa akasema hapana lazima daraja (maegesho) yajengwe, lazima vivuko vipya vijengwe kwa ajili ya wakazi wa Kanda hii ili waendelee kufanya kazi zao vizuri, ni imani yangu kwamba wananchi wataona jinsi Serikali yao inavyowajali.” Kilahala anasema ujenzi wa maegesho hayo ni sehemu ya maandalizi ya kupeleka vivuko vipya vikubwa ambavyo vinaendelea na ujenzi na vinatarajiwa kukamilika hivi karibuni na vitapelekwa kutoa huduma katika maeneo hayo yanayoendelea kuboreshwa.
Wananchi wa Kanda ya Ziwa (Sengerema, Misungwi, Magu, Bunda, Ukerewe) wanasemaje kuhusu huduma za vivuko katika maeneo yao
Wanatoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kwa kuendelea kuwaboreshea miundombinu hiyo ya vivuko ikiwemo majengo ya kupumzikia abiria, maegesho ya vivuko pamoja na ofisi za wakatishaji tiketi za vivuko. Aidha, Wakazi hao pamoja na wafanyabiashara ambao wanatumia usafiri wa mitumbwi kusafrisha bidhaa zao katika baadhi ya maeneo ya Visiwani wanasema vivuko hivyo vipya vitakapowasili watakuwa na uhakika wa kusafirisha mizigo yao kwa urahisi zaidi na usalama zaidi na kuongeza uchumi wao.
Wakazi pia wanasema ujio wa vivuko hivyo utawasaidia watoto wao ambao wanasoma shule zilizoko visiwani na kuhitajika kuvuka maji, wanasema vivuko hivyo vitawasaidia watoto wao kuwa na usafiri wa uhakika tofauti na sasa ambapo inawabidi kutumia mitumbwi kusafiri kutoka kisiwa kimoja kwenda kingine kwa ajili ya kufata huduma mbalimbali za kijami ikiwemo shule na hospitali.
Kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan bado inaendelea na mipango yake ya kuboresha na kuwa na usafiri wa uhakika na imara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kanda ya Ziwa lengo ni kuleta maendeleo na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.