MKUTANO WA SITA WA SEKTA YA UJENZI KATI YA SJMT NA SMZ WAFANYIKA MWANZA

News Image

Posted On: November 11, 2023

Mtendaji Mkuu TEMESA Lazaro Kilahala na timu ya baadhi ya maofisa kutoka Wakala huo leo wameshiriki mkutano wa sita wa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu Sekta ya Ujenzi. Mkutano huo ni muendelezo wa makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi zilizopo chini ya Wizara Ujenzi Tanzania Bara na Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Tanzania Visiwani unajumuisha taasisi za TEMESSA, Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo, Wahandisi na Wakadiriaji Majenzi (AEQSRB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Wajumbe kutoka pande zote mbili wameonesha umuhimu wa ushirikano katika kuendeleza na kuimarisha sekta hiyo ikiwemo usimamizi wa programu zinazohusu wahitimu wa taaluma ya uhandisi nchini na uhamasishaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wanawake ili kuongeza idadi yao.

TEMESA na Wakala wa Karakana Kuu ya Magari Zanzibar (GAWS) wameingia mashirikiano katika kujengea uwezo mafundi na kupeana taarifa kuhusu matengenezo ya magari ambapo taratibu huo utawezesha wataalamu wa pande zote mbili kupata uelewa kuhusu vipuri feki na halisi vya magari kupitia kubadilishana uzoefu, wataalamu na taarifa.

Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort mjini Mwanza na umeongozwa na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Dkt. Khalid S. Mohamed pamoja na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa.