MAENEO HAYA SERIKALI KUYAONGEZEA VIVUKO KUKIDHI HAJA YA USAFIRI

News Image

Posted On: September 17, 2024

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imedhamiria kuboresha na kudumisha utoaji wa huduma za vivuko kote Nchini kwa kuamua kuongeza vivuko vingine vipya kwenye maeneo ambayo tayari yana vivuko lakini vimeonekana kutokutosheleza mahitaji halisi kutokana na kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa miji pamoja na kuzaliana kwa wakazi wa maeneo hayo na hivyo kufanaya idadi ya watu kuongezeka kwa wingi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Ujenzi na Uendeshaji wa Vivuko kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Sylvester Simfukwe wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa kutoka Kitengo cha Masoko na Uhusiano kuelezea mipango ya Serikali katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za vivuko Nchini. Mhandisi Simfukwe amesema kunayo maeneo ambayo yana vivuko lakini Serikali imeona kuna uhitaji zaidi wa vivuko katika maeneo hayo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kunakosababishwa na kukua kwa miji na kukua kwa uchumi.

''Kuna maeneo tuna vivuko ambako tumeona kabisa kwamba huduma inahitajika zaidi ya kile kivuko kilichopo, labda kile kivuko kimeonekana kuwa kidogo kulingana na mahitaji ya watu au watu pia wameongezeka na shughuli za kiuchumi zimeongezeka zaidi, kuna eneo kama Kisorya Rugezi, ambalo linatenganisha Wilaya ya Bunda na Wilaya ya Ukerewe, pale Kisorya Rugezi tuna kivuko kinafanya kazi lakini kile kivuko kina tani 85 ni kidogo, kinabeba abiria 330 na magari madogo 10, eneo hili tunaliongezea kivuko kingine kipya cha tani 170 kwasababu eneo limekuwa na magari mengi yanayoingia na kutoka Wilaya ya Ukerewe kutokana na hali ya huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kukua''. Amesema Mhandisi Simfukwe na kuongeza kuwa ujenzi wa kivuko hicho kipya umefikia zaidi ya Asilimia themanini na kinatarajiwa kupelekwa aeneo hilo ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kulingana na mahitaji ya wakazi wa maeneo hayo.

Mkurugenzi pia ameongeza kuwa eneo jingine ambalo Serikali imeamua kupeleka kivuko kipya baada ya kuonekana kile cha awali hakitosheelezi mahitaji ya wakazi husika ni eneo la Nyakaliro Kome Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema, amesema eneo hilo tayari lina kivuko MV. KOME II ambacho kina uwezo wa kubeba abiria 120 kikiwa na tani 40, kivuko hicho kwa sasa kimezidiwa kutokana na kuongezeka kwa abiria na hivyo Serikali imeamua kupeleka kivuko kipya ambacho kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja kikiwa na tani 170. ''Vivuko vinasaidia sana hivi, miji inakuwa na shughuli za kibinadamu za kiuchumi na za kijamii zinazidi kukuwa kwahiyo watu wanaohitaji huduma ya kuvuka ni wengi kwahiyo pale napo tunapeleka kivuko kipya kabisa, hiki kitaboresha zaidi huduma za uvushaji wa wananchi pale, mizigo na mali zao''. Amesema Mkurugenzi.

Aidha, Mhandisi Simfukwe ameongeza kuwa eneo jingine ambako Serikali inaendelea na ujenzi wa kivuko kipya kabisa ili kuboresha utoaji wa huduma za vivuko ni eneo la Wilaya ya Mafia na Nyamisati Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, amesema eneo hilo lina kivuko MV. KILINDONI ambacho kina uwezo wa kubeba tani 100, lakini Serikali imeonelea kuongeza kivuko kingine kipya ambacho kitakuwa na uwezo wa tani 120 katika eneo hilo ili kiweze kupishana na kivuko kilichopo na kurahisisha huduma za usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo.

''Kuna kivuko kipo pale kina uwezo wa kubeba tani 100 tunaongeza kivuko kingine kipya pale cha tani 120, tunataraji wananchi wa maeneo hayo nao watapata huduma za uhakika kwasababu kila wakati kutakuwa na kivuko cha kuwavusha'', amesema Mhandisi Simfukwe na kuongeza kuwa hizo ndizo juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za uhakika maeneo yote ambayo yanahitaji usafiri ili kuboresha hali zao za kiuchumi.

Mhandisi Simfukwe pia ametaja eneo jingine ambali Serikali pia inaongeza vivuko vipya ni eneo la Magogoni Kigamboni ambapo Serikali inajenga vivuko vidogo viwili (SeaTaxi) ambavyo vitasaidiana na vivuko vilivyopo eneo hilo ili kurahisisha utoaji wa huduma. Ameongeza kuwa kivuko MV. MAGOGONI kinaendelea na ukarabati huko Mombasa Nchini Kenya huku kivuko MV. KIGAMBONI ambacho kimesiama kutoa huduma tayari mkandarasi amepatikana na wakati wowote kuanzia sasa kitaanza kufanyiwa ukarabati mkubwa ili kiweze kurejea haraka kutoa huduma kwa wananchi.

Mhandisi Simfukwe amepongeza juhudi hizo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia kwa Wizara ya Ujenzi katika kusaidia kufanikisha mipango ya Wakala ikiwemo ya miradi ya ujenzi wa vivuko hivyo ambavyo vinakwenda kunufaisha wananchi kwa ujumla.