​SERIKALI YATOA BILIONI 17.8 UJENZI WA VIVUKO VIPYA VITATU MWANZA

News Image

Posted On: January 26, 2023

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 17 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko vipya vitatu Mkoani Mwanza. Vivuko hivyo vitatu, vimeanza kujengwa kwa ajili ya kutumika katika ziwa Victoria katika maeneo ya Ijinga Kahangala Wilayani Magu Mkoani Mwanza, Bwiro Bukondo Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, pamoja na Nyakaliro Kome Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Akizungumza katika hafla fupi ya zoezi la uwekaji wa Msingi wa Kivuko (Keel Laying) iliyofanyika mapema leo katika Yadi ya Songoro iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza, mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa ikiwa ni katika mkakati wa kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na watanzania kwa ujumla na kusema uwekezaji huo utainua hali za kiuchumi na kijamii za jamii zote zitakazonufaika.

‘‘Uzinduzi wa ujenzi wa vivuko hivi vitatu tunaoufanya leo ni hatua muhimu ya kuanza ujenzi rasmi wa Vivuko hivi hivyo niwatake wahusika wote kuhakikisha ujenzi huu unakamilika kwa wakati na viwango vya hali ya juu ili kutimiza azma ya Serikali kuwaondolea kero wananchi na kuwaletea maisha bora.“ Alisema Mhe. Malima na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo mitatu ya Vivuko kwa pamoja.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unaendelea na ujenzi na ununuzi wa vivuko vipya vinane, kati ya vivuko hivyo, vivuko vitano viko kwenye hatua ya ujenzi ambavyo ni Kisorya-Rugezi ambacho ujenzi wake unaendelea, Bwiru-Bukondo, Nyakaliro-Kome, Ijinga-Kahangala, na Mafia-Nyamisati huku mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 33.2 ikiwa tayari imeshasainiwa na wakandarasi wameshalipwa malipo ya awali. Aidha vivuko vitatu vilivyosalia vipo kwenye hatua ya manunuzi na Ujenzi wake unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.

Serikali pia kupitia TEMESA inafanya ukarabati wa vivuko 14 kwa gharama ya shilingi bilioni 22.99 na ukarabati wa miundombinu ya vivuko kwenye maeneo 11 kwa gharama ya shilingi bilioni .4.1 huku mikataba yenye jumla ya shilingi bilioni 60.3 bilioni ikiwa imekwishasainiwa na kazi zinaendelea.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Ludovick Nduhiye ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu Ujenzi akizungumza katika hafla hiyo amesema Vivuko hivyo ambavyo ujenzi wake unazinduliwa leo vimekuwa ni hitaji kubwa kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo vivuko hivi vitaenda kutoa huduma baada ya ujenzi wake kukamilika na hivyo mategemeo ya Wizara ni kwamba wananchi katika maeneo husika watatumia fursa ya kuimarishwa kwa usafiri, kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii ili kuifikia azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala akisoma taarifa fupi ya miradi hiyo amesema kukamilika kwa ujenzi wa vivuko hivyo kutawapatia wananchi wa maeneo ya Nyakaliro Kome, Bwiro Bukondo na Ijinga Kahangala pamoja na wana Mwanza na watanzania kwa ujumla uhakika wa usafiri unaowaunganisha na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli zao za kiuchumi na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali za kijamii kwa haraka zaidi.

Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa kivuko cha Ijinga Kahangala kinagharimu kiasi cha shilingi billioni 5.2 na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100, kivuko cha Bwiro Bukondo kinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.5 na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100 wakati kivuko cha Nyakaliro Kome kinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 8 na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170.

Nao Wabunge wa majimbo ya Buchosa na Ukerewe wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ndani za Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ambayo iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na itawezesha shughuli za kiuchumi za wananchi wa maeneo hayo kutoka kisiwa kimoja Kwenda kingine kuendelea.

Kilahala ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuuwezesha kifedha Wakala kutekeleza miradi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla.