​SERIKALI YAIKABIDHI TEMESA VIFAA VYA SHILINGI MILIONI 545.8

News Image

Posted On: December 20, 2022

Serikali imenunua vifaa vya Umeme na Viyoyozi vyenye thamani ya shilingi milioni 545.8 na kukabidhi kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa TEMESA Tarehe 17 Disemba 2022, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Adelard Kweka, alisema hizo ni jitihada za Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuboresha utendaji kazi wa Wakala huo.

Alieleza matarajio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona vifaa hivyo vinasimamiwa na kutunzwa vizuri, kuongeza tija iliyokusidiwa.

‘’Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kuboresha utendaji kazi wa TEMESA, hivyo watendaji hatuna budi kuendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kuhakikisha vifaa vinatunzwa, vitumike kwa muda mrefu na kuongeza tija.’’ AlisemaMhandisi Kweka na kuahidi Serikali itaendelea kutoa fedha kuhakikisha TEMESA inasimamia na kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Aidha kwa upande wake Mtendaji Mkuu Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala alisema kwa mwaka huu wa fedhaSerikali imetoa shilingi Bilioni 3.9 kukarabati karakana za Mikoa. Alieleza kupitia fedha hizo, wanaendelea na ukarabati wa karakana za Mikoa ya Arusha, Mara, Kigoma, Tabora, Mtwara, Simiyu na Mwanza.

‘’Tunatambua kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi kwa TEMESA kwa sababu ya umuhimu wa shughuli za ufundi zinazotekelezwa, hivyo watumishi tuna wajibu wa kuimarisha ubora wa huduma na kuongeza tija na ufanisi kukidhi matarajio ya Serikali.’’

‘’Kupitia fedha hizi ambazo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa kuboresha huduma, unaahidi kufanya kazi kwa jitihada na weledi wa hali ya juu kufanikisha malengo ya Serikali,’’Alisema Kilahala.

Kilahala pia aliwataka mameneja na wakuu wa vituo vya TEMESA kuhakikisha wanavitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa ufanisi na tija kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alifafanua fedha hizo zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zingeelekezwa kutimiza mahitaji mbalimbali ya Watanzania na kuboresha huduma za afya, elimu na maji, lakini zimeelekezwa TEMESA kwa sababu maalumu.

‘’Serikali inataka kuona TEMESA inaimarika na kuchangia Zaidi katikamaendeleo ya nchi hivyo tunapopokea vitendea kazi hivi pia tulitambue deni tulilonalo kwa Serikali na wananchi kwa kuongeza tija na ufanisi utoaji wa huduma zetu.’’ Alisisitiza.