UONGOZI WA TEMESA WANOLEWA KUPELEKEA TAASISI KUFIKIA MALENGO
Posted On: August 11, 2026
Viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza mafunzo maalum ya uongozi na usimamizi yanayolenga kuwajengea uwezo wa kuongoza kwa weledi, kufanya maamuzi yenye tija na kusimamia rasilimaliwatu kwa ufanisi, kwa lengo la kuifanya TEMESA kuwa taasisi yenye utendaji bora na huduma zinazokidhi matarajio ya wananchi.
Mafunzo hayo yameanza Agosti 10, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Cate Hotel, Morogoro, yakiongozwa na wawezeshaji kutoka Chuo cha Uongozi (UONGOZI Institute), yakiongozwa na Mha. Henry Kulaya na Bwa. Fortunatus Ekklesiah.
Kupitia mafunzo hayo, Viongozi wanajengewa uwezo wa kutazama taasisi kwa mtazamo mpana, kutambua fursa za maboresho, kuhamasisha watumishi na kuongoza mabadiliko kwa namna inayozingatia malengo ya taasisi pamoja na matarajio ya wananchi wanaopokea huduma.
Aidha, Mafunzo hayo yamejikita katika afya ya akili na usimamizi wa msongo wa mawazo mahali pa kazi. Kupitia eneo hili, viongozi wamepatiwa maarifa ya kutambua changamoto zinazoweza kuathiri ustawi na utendaji wa watumishi, namna ya kuzishughulikia kwa busara na kujenga mazingira ya kazi yanayowezesha watumishi kufanya kazi kwa utulivu, weledi na tija.
Mafunzo haya yanayofanyika kwa muda wa siku tatu yanatarajiwa kuwa chachu ya kuibua uongozi unaofikiri kimkakati, unaothubutu kufanya maboresho, unaowekeza kwa watu na unaopima mafanikio kwa matokeo—hatua muhimu katika kuifikisha TEMESA kwenye malengo iliyojiwekea.