​HATMA YA VIVUKO VILIVYOKUWA VIKITOA HUDUMA KATI YA KIGONGO NA BUSISI MWANZA

News Image

Posted On: June 23, 2025

Pengine umeanza kujiuliza maswali mengi sana, nini hatma ya vivuko ambavyo vilikuwa vikifanya kazi katika eneo la Kigongo na Busisi, hatma yake ni nini baada ya uzinduzi wa daraja la JP. MAGUFULI, je bado abiria wataendelea kuvuka kwa vivuko hivyo au watachagua kupita darajani?

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo Juni 19, 2025 alizindua rasmi daraja la JP. MAGUFULI lenye urefu wa kilometa 3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.6. Daraja hilo refu linaunganisha eneo la Kigongo Wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Rais Samia amesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo ni utekelezaji wa ndoto ya hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais Samia amesema kuwa miongoni mwa vitu alivyoahidi ni kuendeleza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wake. Ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo lililoko kwenye barabara kuu ya Usagara-Sengerema-Geita ( Km 90) litachochea uchumi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuunganisha Tanzania na Nchi za DRC. Rwanda, Burundi na Uganda.

Ameongeza kuwa sasa wananchi watatumia dakika 4 tu kuvuka kupitia Daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharamiwa na fedha za ndani ambapo Serikali imetumia Bilioni 718 kukamilisha daraja hilo. “Tanzania sasa inauwezo wa kupanga na kutekeleza miradi yake na asilimia 92 ya wajenzi ni watanzania", amesema Rais Dkt. Samia.Rais Samia amewataka wananchi kulitumia vizuri daraja hilo ili kuongeza tija na kuimarisha biashara za kikanda.

Aidha, Rais Samia amevitaka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na TAROADS kulilinda daraja la J.P. Magufuli ambalo ni la kimkakati na kulifanyia ukaguzi wa mara kwa mara ili lidumu kwa muda mrefu. Vilevile, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kusimamia vizuri ujenzi wa daraja hilo kwa viwango vya ubora.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa miongozo na maelekezo yake yaliyowezesha kukamilika kwa daraja la J.P. Magufuli kwa wakati. "Dkt. Samia alilikuta daraja liko asilimia 25 na fedhq zilizolipwa shilingi Bilioni 152 lakini katika kipindi cha miaka minne amekamilisha ujenzi wote na kulipa fedha zote zilizobakia kwa Makandarasi na Wahandisi Washauri kwa wakati”, Waziri Ulega amesema daraja hilo ni kielelezo cha nchi kufanya uamuzi, kusimamia miradi na kukuza uchumi wa watu wake. Katika kuhakikisha msongamano wa magari unapungua jijini Mwanza Waziri Ulega ameeleza kuwa Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa barabara njia nne kati ya jiji la Mwanza Mjini hadi Usagara (km 22).

Waziri Ulega ameeleza kuhusu hatma ya vivuko vitatu vilivyokuwa vikitoa huduma kati ya Kigongo na Busisi. Vivuko hivyo ambavyo ni MV.SENGEREMA, MV.MWANZA na MV. MISUNGWI vinahamishiwa katika maeneo mengine ya Ziwa Victoria kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma.

Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi Mhandisi Vitalis Bilauri alizungumza na Televisheni ya Taifa TBC na kueleza mahala ambapo vivuko hivyo vinakwenda kutoa huduma baada ya kuondolewa katika eneo la Kigongo Busisi.

Mhandisi Bilauri ameeleza kuwa kivuko MV. MISUNGWI kinatarajiwa kupelekwa kutoa huduma katika eneo la Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza. Eneo hilo kuna kivuko MV. UJENZI ambacho kinao uwezo wa kubeba abiria 330 na magari 10 sawa na tani 85. Kuongezeka kwa wakazi katika maeneo hayo kumefanya kivuko hicho kuzidiwa na uwingi huo wa abiria na hivyo TEMESA sasa itapeleka kivuko hicho ili kikasaidiane na kivuko MV. UJENZI kupunguza adha ya msongamano wanayokumbana nayo abiria wa maeneo hayo.

Eneo jingine ambalo nalo limeonekana kuwa na uwingi wa abiria ni eneo la Nyakarilo na Kome Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, eneo hilo linahudumiwa na kivuko MV. KOME II ambacho kinao uwezo wa kubeba tani 40 pekee, abiria 120 na magari mawili, Serikali imeamua sasa kivuko MV. MWANZA kitapelekwa eneo hilo kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa maeneo hayo ili kuwapunguzia adha ya usafiri waliyokuwa wakikumbana nayo kutokana na udogo wa kivuko walichokuwa nacho. Kivuko MV.SENGEREMA kinatarajiwa kupelekwa eneo la Kanyala kutoa huduma ili kuwarahisishia usafiri wa maji wakazi wa maeneo hayo.

Hiyo ndiyo hatma ya vivuko vilivyokuwa vinatoa huduma katika eneo la Kigongo Busisi.

Daraja la J.P. Magufuli lenye urefu wa kilomita 3 ni Daraja la 7 kwa urefu barani Afrika na la 6 kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.