TEMESA YAFANYA KIKAO CHA WADAU MKOA WA KILIMANJARO NA ARUSHA
Posted On: July 17, 2019
Vikao vya Wadau wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kujadili huduma za wakala na kupata mrejesho wa namna zinavyotolewa vimeendelea wiki hii ambapo maafisa waTEMESA wametembelea mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Katika vikao hivyo ambavyo vimehusisha wadau mbalimbali wa taasisi za umma, taasisi binafsi, wazabuni, pamoja na wauzaji wa vipuri vya magari na mitambo, wadau hao walipata wasaa wa kutoa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kila wakati wanapotumia huduma za Wakala.
Akisoma taarifa ya mapato ya mkoa wa Kilimanjaro, meneja wa TEMESA Mkoa Mhandisi Ferdinand Mishamo alisema mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu walizalisha jumla ya shilingi Bilioni moja milioni mia moja sabini na mbili sawa na asilimia tisini ya lengo ambapo walifanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni moja na kudai shilingi milioni mia nane huku wakidaiwa zaidi ya shilingi milioni mia saba na ishirini na nne ikijumlisha madeni ya miaka ya nyuma.
Nako mkoani Arusha, kikao cha wadau kimefanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi Arusha (Arusha Technical College), Mgeni rasmi wa kikao hicho Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha ndugu David Mwakiposa aliupongeza wakala kwa kuweza kuandaa kikao hicho ili kuweza kupata changamoto na ushauri kutoka kwa wadau inayowahudumia.
Aliushauri wakala kuendelea kutoa huduma bora ili kuendelea kuzivutia taasisi mbalimbali za watu binafsi kuanza kutumia huduma za TEMESA. ''Lazima tutumie huduma za TEMESA na wale waliopewa dhamana hiyo wawe tayari kutoa huduma iliyo bora wakati wote, hiyo itasaidia kuwavutia wale ambao hawatumii huduma zetu'', alisema Katibu Tawala.