WATUMISHI TEMESA WATAKIWA KUTOFANYA KAZI KWA MAZOEA
Posted On: June 06, 2022
Watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini wametakiwa kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ili kuondokana na malalamiko kutoka kwa wateja wake ya kutoridhika na huduma wanayoitoa.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Msaidizi Barabara Kuu (Trunk Roads) Mhandisi Light Chobya aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi Aisha Amour wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Mkuu Mkoani Dodoma.
Mhandisi Light Chobya amesema kuwa malalamiko hayo kutoka kwa wateja wa Wakala yamekuwa yakiutia doa Wakala hivyo yanapaswa kushughulikiwa mapema iwezekanavyo.
‘’Yapo malalamiko kutoka kwa wateja wenu kuhusu huduma mnazozitoa, mathalani, ucheleweshaji wa matengenezo ya magari, matengenezo ya magari yasiyokuwa na viwango, gharama za matengenezo kuwa kubwa, vipuri visivyo halisi na kadhalika.’’ Alisema Mhandisi Chobya.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala, Lazaro N. Kilahala, akizungumza katika mkutano huo, amezitaja baadhi ya changamoto zinazoukabili Wakala huo ikiwemo gharama kubwa za uendeshaji wa vivuko kutokana na Wakala kutegemea watumishi wa mkataba kwa zaidi ya asilimia 80%, kupanda kwa gaharama za mafuta na vipuri, pamoja na tozo za nauli za vivuko ambazo zimepitwa na wakati, Mtendaji Mkuu pia amezungumzia tozo ya faini ambayo Wakala umetozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao unaugharimu wakala takribani shilingi milioni 102 kila mwezi.
Aidha Mtendaji Mkuu alitaja mikakati ambayo TEMESA imejipanga kuitumia ili kukabiliana na changamoto inazokutana nazo katika shughuli zake za kila siku za kiutendaji ambapo alisema, ‘’Tutaongeza ufanisi na tija katika utendaji, tutateua wazabuni wachache wenye mitaji mikubwa na uwezo wa kutuuzia Wakala vipuri halisi kwa bei nafuu na kwa haraka na kuongeza udhibiti wa matumizi katika vivuko hasa eneo la mafuta’’. Alimaliza Mtendaji Mkuu.
Mkutano huo pia ulipitia muhtasari wa kikao cha Baraza la wafanyakazi kilichofanyika mwaka 2021, ulipitia maazimio ya Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la mwaka 2021 pamoja na kupitia na kusoma makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha ujao wa 2022/2023 ambapo TEMESA imepanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 123,431,429,030.