TEMESA YAZIOMBA TAASISI ZINAZODAIWA KULIPA MADENI YAO
Posted On: October 29, 2022
Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA umeziomba Taasisi ambazo unazidai kulipa madeni ili wakala huo uweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi na hivyo kufikia matarajio yake. Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro Kilahala Tarehe 28 Oktoba katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Ramada iliyoko Mbezi jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa mpango kazi kati ya TEMESA, wadau inaowahudumia ikiwemo Taasisi za Serikali pamoja na wazabuni wanaofanya kazi na Wakala huo. Kilahala ameeleza kuwa kwa sasa Wakala umeamua kufanya mabadiliko makubwa.
‘’Mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu madeni yalikuwa takribani Bilioni 43 ambayo tunawadai wateja wetu mbalimbali, wateja wetu ni Taasisi mbalimbali za Serikali, lakini na sisi pia tunadaiwa, madeni ya takribani bilioni 42,kutoka kwa wazabuni mbalimbali ambao tunafanya nao kazi kwahiyo unaona hali inakuwa ngumukwetu kuweza kutoa huduma bora Zaidi wakati wale tunaotegemea watupatie vifaa nao wanatudai madeni makubwa’’, alisema Mtendaji Mkuu.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho ameuomba Wakala huo kuhudumia kwa welediTaasisi zote zinazopata huduma kutoka TEMESA. ‘’Naomba niseme kwamba kumekuwa na malalamiko ya wadau wengi kwamba magari yakienda TEMESA yanakaa muda mrefu, tayari umeshazungumza kwamba malalamiko hayo yamekuja na yanafanyiwa kazi’’, Alisema Mkuu wa Wilaya na kuongeza kuwa hapo awali kumekuwa na malalamiko kwamba kuna mlolongo mrefu wa vipuri kupatikana kutokana na mlolongo wa manunuzi na gari ikikaa pale muda mrefu kwa namna yoyote ile mambo mengine yanaweza kutokea kule ndani yake ikiwemo kupotea kwa baadhi ya vipuri au kuharibika Zaidi kwa gari husika.
Naye Meneja wa TEMESA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Liberatus Bikulamchi akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kikao hicho amesema karakana ya TEMESA Mkoa ya Vingunguti imeanza kufunga mifumo ya gesi kwenye magari ikiwa ni mbadala wa mafuta ya diseli na petroli, ‘’changamoto iliyopo ni kwamba hatuwezi kuituliza bei ya mafuta inayopanda kila kukicha kidunia lakini kingine kikubwa ni kwamba tuna fursa ya gesi hapa Tanzania sasa tumekuja na hiyo teknolojia ya ambayo tunaweza tukabadili mifumo ya gari badala ya gari kutumia petroli ikatumia gesi kabisa lakini vile vile gari ikatumia sehemu ya mafuta ya petroli au diseli pamoja na gesi. Alimaliza Mhandisi Bikulamchi.