TEMESA YAANZA RASMI KUTUMIA MFUMO WA KADI KIVUKO CHA MAGOGONI
Posted On: March 02, 2022
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) hatimaye umeanza rasmi kutumia mfumo mpya wa kadi na kuachana na mfumo wa zamani wa kutumia risiti za mashine maarufu kama (POS) ambazo zilikuwa zikitoa risiti za karatasi. Mfumo huo mpya ambao ulianza kwa majaribio kuanzia mwishoni mwa mwaka 2020 unachukua rasmi nafasi katika kivuko hicho na unatarajiwa kufungwa katika vivuko kote nchini ifikapo baadae ili kuachana kabisa na mfumo wa karatasi.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya mwisho ya kutumia mfumo wa risiti za karatasi, meneja wa Ujenzi na Uendeshaji wa vivuko Mhandisi Lukombe King'ombe amesema kuwa mfumo huo unasaidia kuondoa msongamano na kuwarahisishia abiria kuvuka kwa wakati tofauti na mfumo wa zamani ambapo iliwabidi abiria kuanza kukata tiketi kwa misururu na baadae kupanga tena foleni ili kupita katika mageti kabla ya kuingia kwenye kivuko.
Mhandisi King'ombe amesema kuwa kadi za kutumia kivukoni hapo zinapatikana kwa shilingi elfu moja na zinapatikana kivukoni hapo kupitia kwa maafisa wa NIDC ambao wanapatikana kivukoni hapo.
Kuhusu wageni ambao wanaenda kuvuka kivukoni hapo mara moja moja, Mhandisi King'ombe amesema wameandaliwa utaratibu maalumu ambapo watapata kadi kwa shilingi mia mbili na kuna mashine zimetengwa kwa ajili yao ambapo wataingiza kadi hiyo ndani ya mashine hiyo na geti kufunguka.
Mfumo huo mpya wa kidigitali unatarajiwa kuepusha upotevu wa mapato kwa kiasi kikubwa kwani pesa sasa zitakuwa zinakatwa kidigitali bila kupita mikononi kwa mtumishi yoyote.