TEMESA TRA ZAINGIA MAKUBALIANO MATENGENEZO YA MAGARI

News Image

Posted On: April 27, 2023

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA umeingia makubaliano ya kiungwana (Memorandum of Understanding) na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa lengo la kuboresha huduma za matengenezo ya magari, kangavute pamoja na vyombo vingine vya moto. Makubaliano hayo yameingiwa na pande zote mbili ili kuhakikisha vyombo vya Mamlaka ya Mapato Tanzania vinapata huduma nzuri, vipuri vyenye ubora unaostahili, huduma ya haraka na ya muda mfupi ili kuiwezesha Mamlaka hiyo kutimiza majukumu yake ya ukusanyaji na ufuatiliaji wa Kodi kwa uharaka.

Kikao cha kurejea makubaliano baina ya pande hizo mbili kimefanyika leo katika hoteli ya Oasisi iliyopo barabara ya Stesheni Mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na viongozi kutoka Mamlaka hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Moshi Kabengwe na baadhi ya viongozi kutoka menejimenti ya TEMESA. Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda ameishukuru Mamlaka hiyo kwa kukubali kuingia makubaliano hayo na kuwahakikishia kwamba Wakala umejipanga na utatimiza makubaliano hayo kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuiwezesha Mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake ya ufuatiliaji na ukusanyaji wa Kodi kwa uhakika zaidi. Kikao hicho pia kimejadili rasimu za makubaliano ya kiwango cha huduma na kuazimia kwa pamoja makubaliano hayo.