TEMESA KUFUNGA KAMERA ZA ULINZI KUILINDA KARIAKOO MASAA 24
Posted On: February 20, 2025
Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam imesaini mkataba na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unaogharimu sh.Milioni 514 za uwekaji wa mifumo ya kamera za ulinzi (cctv cameras)katika barabara na maeneo ya Kariakoo ili kuimarisha ulinzi pindi biashara zitakapokuwa zinafanyika saa 24.
Akizungumza wakati wa halfla ya utiaji saini mikataba zaidi ya mitatu ya miradi mbalimbali iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee Februari 18,2025, Mkurugenzi wa Jiji hilo Elihuruma Mabelya amesema hatua hii ina lengo la kudhibiti vitendo vya uhalifu na kusaidia vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mkurugenzi huyo amesema ufungaji wa kamera hizo utaongeza wigo wa wafanyabiashara kukuza mitaji yao kutokana na kuweza kufanya biashara zao nyakati zote bila kuhofia usalama wao na mali zao.
"Lengo la Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni wafanyabiashara wafanye biashara zao usiku na mchana,lakini haya yote hayawezi kufanyika kama wafanyabiashara hawatakuwa na uhakika wa ulinzi na usalama". Alisema Mabelya.
Aidha Meneja wa Kikosi cha Umeme TEMESA, Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema mkataba huo unahusisha ufungaji wa kamera 40 za awamu ya kwanza, usimikaji wa chumba cha uendeshaji (control room) chenye uwezo wa kubeba kamera zaidi ya 1000, usimikaji wa mfumo wa kubeba taarifa kutoka mwenye kamera na kuzipeleka kwenye chumba cha uendeshaji (control room) na usimikaji wa mfumo wa kupeleka umeme kwenye kamera kutoka kwenye chumba cha uendeshaji (control room).