TEMESA TANGA YAALIKA WADAU KUSIKILIZA KERO ZAO
Posted On: July 11, 2019
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Tanga jana umealika wadau wanaotumia huduma zake ili kujadilli na kupata mrejesho kuhusu namna zinavyotolewa. Kikao hicho cha wadau kilichoandaliwa na meneja wa mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina kilifanyika katika eneo la wazi la karakana ya wakala huo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa na wadau mbalimbali wa taasisi za umma, taasisi binafsi, wazabuni, pamoja na wauzaji wa vipuri vya magari na mitambo.
Awali, Akifungua kikao hicho, meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga alisoma taarifa ya utendaji kazi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo taarifa hiyo imeonyesha kiwango kikubwa cha ukuaji wa uzalishaji ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu uzalishaji wa mkoa huo umeweza kufikia zaidi ya shilingi Bilioni moja nukta tano sawa na asilimia tisini nukta nne ya uzalishaji wa mkoa.
Mhandisi Margareth alizungumzia pia changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ikiwemo kucheleweshewa malipo ya madeni wanayodai wateja hasa wa Umma, ‘’hadi kufikia Juni mwaka 2019 tunadai zaidi ya shilingi milioni mia sita, tunaendelea na usuluhishi wa madeni hayo na wateja wetu ili kuingiza deni sahihi katika taarifa zetu za fedha za mwaka,’’alisema.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle alieleza mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika Wakala ambapo huduma za karakana zimeanza kusogezwa kwa wateja wa mbali hasa uanzishwaji wa karakana mpya za Wilaya ikiwemo uanzishwaji wa karakana ya TEMESA katika Halmashauri ya mji wa Ifakara ambayo tayari imekwishaanza kufanya kazi,
‘’TEMESA imeanza kubadilika, tuna mpango wa kuanzisha karakana katika Wilaya ya Same, Wilaya ya Simanjiro, Wilaya ya Korogwe pamoja na Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, tumesambaza vifaa vipya vya kisasa kwa ajili ya karakana kumi na mbili na tayari vingine vipo kwenye mchakato wa manunuzi’’. Alisema Mhandisi Maselle.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa alimshukuru meneja kwa kumkaribisha kwenye kikao hicho kama mdau, pia aliipongeza TEMESA kwa ubunifu na hatua wanazochukua kutatua kero za wateja wao ambapo alisema malalamiko mengi kwa sasa yamepungua tofauti na hapo awali ambapo akiwa Wilayani Manyara malalamiko yalikuwa mengi sana na kwa sasa hayapo tena.
Nao baaadhi ya wadau walizungumzia kero zinazowakabili ikiwemo kucheleweshewa matengenezo ya magari, gharama kuwa juu pamoja na upungufu wa vipuri. Pia wadau hao waliomba mafundi wa karakana wapewe elimu ya kumhudumia mteja kwani wengi wao wamekuwa na kauli ngumu kwa wateja wao.
Akijibu malalamiko hayo Mtendaji Mkuu alisema kucheleweshwa kwa matengenezo ni kutokana na kukosekana kwa vipuri katika karakana husika lakini tatizo hilo limekwishatatuliwa kwa kuwa sasa Mkoa wa Tanga una akiba ya kutosha ya vipuri, aliongeza kuwa Wakala sasa unaanzisha huduma ya kuhudumia wateja maarufu ambapo kipaumbele kitatolewa kwa wateja hasa wa magari ya viongozi ikiwemo wakuu wa Wilaya, wakuu wa Mikoa pamoja na Mawaziri ambao magari yao yatakuwa yakipatiwa huduma ya haraka pindi yanapofika katika karakana husika. Kikao kingine cha wadau kinategemewa kufanyika mkoani Kilimanjaro pamoja na mkoani Arusha siku ya Ijumaa.