TEMESA YAANZA KUFANYIA KAZI MALALAMIKO YA WATEJA
Posted On: March 21, 2024
Wakala Wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umeanza kufanyia kazi malalamiko ya wateja wake, ambao wengi walilalamikia gharama kubwa za matengenezo ya magari, pamoja na matengenezo yasiyofikia viwango. Malalamiko mengine yalikuwa ucheleweshaji wa matengenezo, uwepo wa mafundi wasiokuwa na uwezo, na uadilifu, uhaba wa vipuli, pamoja na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha.
Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi (TEMESA), Hassan Karonda ameyasema hayo Tarehe 15 Machi 2024 wakati alipomwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wakati wa kikao cha wadau wa TEMESA Mkoa wa Simiyu. Karonda amesema kuwa kuhusu changamoto ya gharama za matengenezo, TEMESA imeingia mkataba na wazabuni zaidi ya 56 kwa ajili ya kutoa huduma ya vipuli pamoja na vilainishi kwa gharama nafuu.
“ Gharama kubwa ambazo wateja wetu walikuwa wanalalamikia asilimia 70 zilitokana na vipuri na vilainishi, katika mkakati wetu mpya tumeingia mkataba na wazalishaji moja kwa moja wa bidhaa hizo ambazo wanatupatia kwa gharama nafuu,” Amesema Karonda. Kuhusu mafundi wasiokuwa na ujuzi, weledi na uadilifu, Mkurugenzi huyo alisema kuwa wameingia mkataba na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa ajili ya kuwapatia mafundi wenye ubora ujuzi wa kutosha.
“ Karakana zetu zote nchi nzima tumefunga kamera za CCTV ili kukomesha wafanyakazi wasiokuwa na weledi na uadilifu na mpaka sasa zaidi ya watumishi 7 wakiwemo mafundi wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi katika mikoa ya Dodoma na Kigoma,” alieleza Karonda. Ameongeza kuwa mbali na hilo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka huu wa fedha imetoa kiasi cha Sh milioni 700 kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi lengo likiwa kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Bi. Anna Gidalya alizitaka taasisi zinazodaiwa na TEMESA kuhakikisha zinalipa madeni yao kwa wakati ili kuiwezesha TEMESA kutekeleza majukumu yake ipasavyo.