WADAU TEMESA RUKWA WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO KIDIGITALI WA USIMAMIZI WA KAZI ZA MATENGENEZO (MUM)
Posted On: May 06, 2025
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeendelea na utoaji wa mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM)kwa watumishi wa taasisi mbalimbali mkoani Rukwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma kwa zitolewazo kwa wateja wake kwa kutumia mfumo wa kidijitali unaoendana na zama za sasa.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Mratibu wa Mafunzo ambaye pia ni Meneja wa TEMESA mkoani Mbeya, Mhandisi Clement Abadyame, na yamehudhuriwa na watumishi kutoka taasisi za serikali, washitiri pamoja na watumishi wa TEMESA mkoani humo.
Katika mafunzo hayo, Mhandisi Abadyame ameeleza kuwa mfumo wa MUM umebuniwa ili kurahisisha ufuatiliaji wa kazi za matengenezo, kuongeza uwajibikaji, na kuhakikisha huduma zinazotolewa na TEMESA zinaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.
"Kupitia mfumo huu, tunatarajia kuona ongezeko la ufanisi katika utendaji kazi na usimamizi wa mali za umma. Maoni ya washiriki ni muhimu sana katika kuendelea kuuboresha mfumo huu,”alisema Mhandisi Abadyame.