WADAU WA TEMESA MWANZA WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA USIMAMIZI WA KAZI ZA MATENGENEZO (MUM)
Posted On: April 23, 2025
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania umeendelea kuendesha mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi kutoka taasisi za serikali kuhusu matumizi ya mfumo huo wa kidijitali.
Mafunzo hayo, yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Adden Palace Hotel na kuwakutanisha pamoja Maafisa Usafirishaji kutoka taasisi mbalimbali za serikali Mkoani Mwanza, pamoja na wawakilishi wa karakana teule zilizosajiliwa na TEMESA.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Kikosi cha Umeme ambaye pia ni Mratibu wa Mfumo huo, Mhandisi Pongeza Semakuwa amewasihi washiriki kuunga mkono jitihada za serikali katika kuleta mabadiliko ya kidijitali kwa lengo la kuboresha huduma za TEMESA kwa umma.
“Mfumo huu wa MUM ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendeshwa na serikali katika kuhakikisha TEMESA inatoa huduma bora, kwa uwazi na kwa wakati. Ushiriki wenu kama wadau ni muhimu sana katika kufanikisha azma hiyo”, alisema Mhandisi Semakuwa.
Naye Meneja wa mkoa wa mwanza amesema mfumo huu ni shirikishi kwa wadau wote ili uweze kurahisisha majukumu, kupunguza gharama , muda lakini pia unampa mteja uhuru wa kuomba huduma anayohitaji mahali popote kwa njia ya mtandao.
Kwa upande wa Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa kwao na hatua ya TEMESA kuwawezesha kwa kuwapatia ujuzi wa kutumia mfumo wa MUM, wakisisitiza kuwa mfumo huo utarahisisha kazi zao za kila siku.