​‘’MABADILIKO TEMESA YASIWE YA NDANI TU, WA NJE PIA WAYAONE,’’ ASEMA NAIBU WAZIRI KASEKENYA

News Image

Posted On: July 17, 2026

Naibu Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa. Mhandisi Godfrey Kasekenya ameuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuhakikisha mabadliko unayoyatekeleza yanaonekana kuanzia ndani ya taasisi mpaka nje ya taasisi kwa wadau wanaopokea huduma kutoka kwao. Mhe. Naibu Waziri ameyasema hayo leo tarehe 17 Julai 2026 alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za TEMESA Makao Makuu jijini Dodoma.

Mhe. Mha. Kasekenya amesisitiza kuwa TEMESA ni moja ya taasisi nyeti na za kimkakati Nchini na ndani ya Wizara ya Ujenzi kutokana na mchango wake mkubwa katika utoaji huduma za ufundi, umeme, matengenezo ya magari, ukodishaji mitambo na vivuko. Akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa TEMESA, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Mha. Kasekenya amesema watumishi wanatakiwa kufanya kazi kwa umoja ili kufikia malengo.

''Kama mnataka kuleta mageuzi TEMESA mnatakiwa kufanya kazi kama timu, mnatakiwa kama viongozi muwahamasishe hawa watumishi na mtumishi yoyote anapofanya kazi vizuri, tuangalie namna ya kumtambua na kumpa motisha. TEMESA ni moja ya Taasisi ambazo katika Nchi hii na katika Wizara ya Ujenzi ni nyeti’’. Amesema Mhe. Mha. Kasekenya na kuongeza kuwa TEMESA ina mchango mkubwa sana katika kuleta mageuzi hapa Nchini. Mhe. Mha. Kasekenya ameongeza kuwa wao kama Wizara wanatamani watumishi pia wahusishwe na waone umuhimu wa kubadilika na kama walikuwa wanaweza kutengeneza magari kumi basi sasa wanaweza kutengeneza magari zaidi ya hayo.

Aidha, Naibu Waziri wa Ujenzi amempongeza Mtendaji Mkuu kwa kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa mabadiliko ambayo ameendelea kuyasimamia na kusema wao kama Wizara wangetamani TEMESA ibadilike irudi kwenye mstari wake ishike kazi zake ambazo ziko kisheria na watumishi watimize wajibu wao ili washitiri waje kupata huduma si kwa sababu ya kisheria bali waje kwa sababu TEMESA inatoa huduma bora na si vinginevyo.

‘’Mtendaji Mkuu nikupongeza sana kwa kuteuliwa kushika nafasi hii. Na watumiaji nadhani dhamira ya Mtendaji Mkuu mnaiona kabisa anataka kuijenga taasisi sasa hata kama utasema unataka kwenda taasisi nyingine ukumbuke kuwa ile ilijengwa na sasa kwa hapa kwenu wewe ndo wakuijenga tasisi yako ili pia itamaniwe, kama unapata mafunzo jua kwamba tunakupatia mafunzo ili uje kuisaidia taasisi hii. Tunataka mjenge taasisi ambayo ina nguvu, taasisi ambayo inaheshimika na yenye hadhi, taasisi ambayo watu watasema mimi gari yangu lazima iende TEMESA,tuwe na mitizamo ya kiushindani na tujione kama ni shirika ama taasisi ya umma ambayo ina shindana na taasisi binafsi, sisi tunachohitaji TEMESA msimame na mtoe huduma bora kwa watanzania”.

Naye Mtendaji mkuu TEMESA Bw. Kheri A. Mahimbali akizungumza katika kikao hicho amesema TEMESA ilipewa malengo mbalimbali ya makusanyo imeweza kufanya bidii kubwa katika makusanyo hayo na kupita malengo iliyowekewa na Serikaili.

‘’Tunakusanya kwa kiasi kikubwa kabisa kama ambavyo wasilisho limesema, ambapo kuna mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani na makusanyo mengine ni fedha kutoka Serikali Kuu’’. Amesema Mahimbali na kuongeza kuwa TEMESA imejipanga kukusanya zaidi ya mara dufu kuliko lengo ambalo imewekewa.

“Tunakusudia mwaka huu wa fedha kukusanya vizuri zaidi ya mwaka uliopita kwasababu tunataka tukaboreshe kwenye baadhi ya maeneo mfano mitambo, karakana umeme na vivuko ambako kutaboresha makuaanyo yatayopelekea kuboresha maalahi ya watumishi wetu, alimaliza Mahimbali.

Ziara hiyo ya kikazi ilikuwa sehemu ya usimamizi endelevu wa Wizara kuhusu utekelezaji wa mageuzi ya kimkakati ndani ya TEMESA, yaliyolenga kuboresha ufanisi wa kiutendaji, utoaji wa huduma, na mchango wa Wakala katika ajenda ya maendeleo ya taifa.