TEMESA YAWAPATIA MAMENEJA WAGAVI NA WAHASIBU MAFUNZO MFUMO WA MADENI

News Image

Posted On: March 21, 2023

Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Bi. Josephine Matiro leo amefungua mafunzo kwa wahasibu, wagavi pamoja na Mameneja wa Mikoa. Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Wakala huo yaliyopo maeneo ya Tambukareli mjini Dodoma na yamejikita katika ajenda mbili, ambayo ya kwanza nikuingiza madeni kwenye mfumo wa madeni wa TEMESA pili ni kuwafundisha mfumo wa manunuzi (Purchase Module).

‘’Tumeanzisha mfumo wa madeni ambao tunataka uingie kwenye mifumo yetu, Wakala umeona umuhimu wa kufanya zoezi hili, tunatambua kwamba mafunzo yalikuwa yameshaanza kwa Mikoa kumi lakini tumeona kwa sababu ya muda na taarifa hizi zinatakiwa wale wahusika wote tuwaite ili waweze kujifunza mfumo huu na watakuja watu wengine kuwafundisha ili kila mmoja wetu anakorudi akalifanyie kazi suala hili akiwa ana uelewa wa pamoja. Mkurugenzi ameongeza kuwa faida za mfumo huo ni madeni kusomeka kwa usahihi bila kutofautiana Mikoani pamoja na Makao Makuu. Mfumo huo pia unasaidia nyaraka pamoja na viambatisho vyote vya deni husika kuwa kwenye mfumo.

‘’Mimi niwaombe tu, kwamba tumekuja hapa kwenye kikao kazi, kazi yetu ni kwenda kuingiza madeni yetu kwenye mfumo, madeni haya, taarifa hizi zinatakiwa zinasubiriwa na viongozi wetu, mkirudi naomba mlipe hili suala kipaumbele kwasababu ni kitu ambacho kinasubiriwa pande zote’’Alimaliza Mkurugenzi.

Mafunzo hayo ya siku moja yanatarajiwa kufungwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro Kilahala.