TEMESA YAZIDAI TAASISI ZA SERIKALI BIL.1.8 MATENGENEZO YA MAGARI
Posted On: March 28, 2024
Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) Mkoani Tanga umesema unazidai taasisi za Serikali madeni sugu ya zaidi ya sh. Bilioni 1.8.
Umesema fedha hizo walikwenda kutengeneza magari yao katika karakana ya wakala huo ambapo mengine ni ya muda mrefu.
Hayo yamesemwa Jana na Meneja wa TEMESA Mkoani Tanga Jairos Nkoroka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema wanaziomba taasisi hizo kulipa madeni yao ili kuuwezesha wakala huo kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi.
Meneja huyo pia aliziomba taasisi hizo ziweze kulipa madeni yao kutokana na kwamba wanadaiwa sh. Bilioni 1.4 na wazabuni ambao wamekuwa wakipeleka vifaa kwa ajili ya kutengeneza magari.
“Tunawakumbusha watulipe ili tueweze kuwapa huduma kwani kutokufanya hivyo kunaweza kusababisha kutokupata huduma kwa wakati”, alisema.
Aidha alisema kwamba madeni mengi ni ya nyuma ambayo wameyarithi na mengine wameyapeleka makao makuu yao kwa utaratibu mwingine na mwaka huu wanaendelea kuwadai kuhakikisha wanawalipa.
“Tumeanzia kitengo cha mahusiano kupitia mabalozi kwa kujenga mahusiano na hivyo kusaidia wanaodaiwa kuanza kulipa madeni yao na tunaamini tunaendelea kupata mafanikio”, alisema.
Aidha alisema ili kuweza kukabiliana na wadaiwa hao sugu TEMESA imeingia mkataba na wazabuni wakubwa arobaini (40) wa vipuri vya magari Mkoani Tanga ili kuondoa ucheleweshaji ambao ulikuwepo awali badala ya kuanza taratibu za manunuzi ambazo siku za nyuma zilikuwa zinachelewesha.
Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha wanaondokana na ucheleweshwaji na kwa sasa wanachukua mda mfupi baada ya siku mbili.
“Hivi sasa tumeingia mkataba na wazabuni wakubwa na matengenezo ya magari ya Serikali yanatakiwa kutengenezwa na TEMESA na tukishindwa kutengeneza kutokana na sababu za kitaaluma au vifaa kama utaratibu ambao unafahamika na tunatoa vibali kwenda kwenye karakana nyingine, na yanatengenezwa chini ya usimamizi wao”, alisema.